Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Korogwe
SERIKALI imesema elimu ya lazima sasa itakuwa ni kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne, huku walimu watakaofundisha shule za msingi watatakiwa wawe wamemaliza kidato cha sita na kuweza kubobea kwenye masomo watakayofundisha.
Hayo yamesemwa Novemba 25, 2024 na Mkurugenzi wa Mafunzo ya Ualimu nchini kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,Huruma Mageni wakati anazindua vitabu vya kiada kwa walimu tarajali katika Chuo cha Ualimu Korogwe mkoani Tanga.
Mageni amesema mabadiliko hayo ya mitaala pia yanawagusa walimu, kwani zamani walimu walikuwa wana uwezo wa kufundisha masomo yote, lakini baadae ilikuja ikabaini sio kweli. Hivyo, mitaala ya sasa itamtaka mwalimu afundishe masomo aliyobobea, na yasiwe zaidi ya mawili. Hivyo walimu watatakiwa kuongeza kiwango chao cha elimu.
“Kwenye huu mtaala ulioboreshwa, mwalimu anaetaka kufundisha shule ya msingi ni lazima awe amemaliza kidato cha sita, na sio Form Four (kidato cha nne) kama zamani. Na ukimaliza kidato cha sita uende kusomea ualimu kwenye masomo uliyobobea kwenye kidato cha sita, na tunataka masomo mawili tu uliyobobea.
“Lakini kwa walimu watakaofundisha sekondari watatoka vyuo vikuu. Vyuo vikuu vyote wameshaelekezwa kutokana na mitaala iliyoboreshwa ili waende wakawaandae walimu wao kupokea haya mabadiliko. Hivyo, kupitia mabadiliko hayo tunaamini elimu yetu inakwenda kuwa nzuri sana nchini, na hiyo itaondoa dhana iliyojengwa zamani kuwa mtu akikosa kazi anaulizwa, umeshindwa hata kusomea ualimu!” alisema Mageni.
Mageni amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imeweka historia adhimu katika vyuo vya ualimu hapa nchini kwa kuwa na kitabu cha kiada kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa Elimu ya Ualimu.
“Leo tunazindua, uzinduzi wa vitabu vya kiada kwenye vyuo vyetu vya ualimu nchini. Kutokana na mabadiliko ya Sera na Mtaala ya mwaka 2014 toleo la 23. Wote tunafahamu kwamba, Serikali ilichukua maamuzi sahihi kabisa yaliyoongozwa na Jemedari wetu Mkuu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwani yeye mwenyewe kwa utashi wake alipoingia madarakani tu, alisema anahitaji kufanya maboresha ya mtaala wetu Tanzania.
“Na mtaala wetu hasa alisema ni vizuri ukalenga kwenye kujiandaa vijana wetu kwa kujitegemea au kujiajiri, hivyo ikabidi mtaala uliopo upitiwe, na mtaala wetu wa sasa wote mnaufahamu. Tukianza na elimu ya msingi, sasa itakomea darasa la sita na sio la saba tena. Watasoma darasa la awali mwaka mmoja halafu msingi miaka sita. Na baadae wataenda sekondari ya chini kwa miaka minne, hivyo elimu ya lazima kwa wanafunzi wote wanaoanza darasa la kwanza itakwenda hadi kidato cha nne, na sio darasa la saba kama zamani” alisema Mageni.
Mageni alisema baada ya hapo wanafunzi watakwenda kwenye makundi mbalimbali. Kuna watakaokwenda kidato cha tano na sita, na wengine kwenye vyuo vya ufundi. Lakini baada ya elimu ya msingi, kuanzia kidato cha kwanza kutakuwa na mikondo miwili mikubwa. Mkondo wa kwanza ni ule wa jumla kama wanavyosoma sasa, lakini mkondo wa pili ni Amali ambao kwa sasa ndiyo kipaumbele kwa nchi yetu.
“Mafunzo ya Amali ndiyo kila kitu. Ukiangalia nchi zilizoendelea duniani, ziliwekeza kwenye amali, kwani watu wote wenye ujuzi wanazalishwa kwenye vyuo vya amali. Hivyo, mafunzo ya amali ndiyo kipaumbele cha sasa hapa nchi, na leo tunazindua vitabu kwa ajili ya vyuo vya ualimu hapa nchini, lakini pia tunazindua vitabu kwa ajili ya elimu ya amali kwa sekondari hapa nchini” alisema Mageni.
Akisoma taarifa, huku akipokea vitabu akiwakilisha vyuo vyote 36 vya ualimu vya Serikali nchini, Kaimu Mkuu wa Chuo cha Ualimu Korogwe Beatrice Nimrod, alisema anaishukuru Serikali kwa kuwapatia mtaala, mihutasari, na vitabu vya kiada vya mtaala ulioboreshwa katika ngazi ya elimu ya msingi kwa madarasa ya awali, darasa la kwanza na la tatu, na mtaala wa shule za msingi darasa la kwanza hadi la sita vyenye thamani ya sh. 4,678,401.
“Mtaala, mihtasari na vitabu tulivyopokea ni kwa ajili ya tahasusi ya sayansi kwa shule zinazotumia lugha ya Kiswahili na Kiingereza kufundishia katika elimu ya msingi kwa mtaala ulioboreshwa. Vile vile tunawashukuru Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kuandaa mtaala wa Elimu ulioboreshwa, na uwepo wetu mahali hapa ni matokeo ya kazi yao.
“Chuo cha Ualimu Korogwe kwa niaba ya vyuo 36 vya ualimu vya Serikali nchini, tunaahidi kusimamia matumizi ya vitabu hivyo, kwa kuhakikisha wanachuo wetu pamoja na wakufunzi wanavitumia kikamilifu katika ufundishaji na ujifunzaji.
More Stories
Kamati ya Mfuko wa Jimbo Musoma Vijijini yagawa vifaa vya ujenzi
Hatma mrithi wa Kinana kupatikana
Mrithi wa Kinana CCM kujulikana katika Mkutano Mkuu wa Jan 18/19