April 30, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Walimu Bagamoyo wafanya ziara Shule ya Msingi Olympio

Na Heri Shaaban, TimesMajira Online

Walimu Wakuu 42 wa Shule za Msingi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo wamefanya ziara ya kimafunzo katika Shule ya Msingi Olympio yenye lengo la kujifunza mbinu za kufundisha na masuala mengine muhimu yatakayowawezesha kupandisha kiwango cha ufaulu wilayani Bagamoyo .

Akiongea katika mafunzo hayo, Afisa Elimu Taaluma Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo Mwalimu Joseph Bureta alisema wameichagua Shule ya Msingi Olympio kwani ni Shule ya Serikali inayofanya vizuri kitaaluma katika ngazi ya Wilaya, Mkoa na Taifa na kumshukuru Mwalimu Mkuu kwa mapokezi mazuri.

“Lengo la kuja shuleni hapa ni kujifunza namna ya kuongoza shule na namna ya kusimamia mikakati ya kuinua taaluma katika Wilaya ya Bagamoyo. Tumeona jinsi walimu wanavyojituma na kuwasimamia wanafunzi licha ya kuwa na wanafunzi wengi lakini hali ya mazingira ni safi na utulivu wa wanafunzi wanalidhisha “alisema Mwalimu Bureta.

Mwalimu Bureta alisema ana imani kuwa mafunzo hayo waliyopata hapa walimu alioambatana nao wataitendea kazi na kuleta mabadiliko chanya ya kitaaluma katika Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani.

Aidha, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Olympio Mwl. Reuben Mduma Gadi alisema ”Tunayo furaha kuwakaribisha Walimu Wakuu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo waliokuja kujifunza baada ya kuona shule yetu ina mafanikio kitaaluma miaka mitatu mfululizo. Lakini sisi kama Shule ya Olympio tumepata mengi kutoka kwao ambayo yatatusaidia kuboresha zaidi ufundishaji kwenye shule yetu.”

Sambamba na hilo amesema “Namshukuru Rais Wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani aametusaidia kuhakikisha miundombinu ya shule inakua katika hali nzuri na uhakika wa upatikanaji wa vitabu shuleni, na kusaidia kwenye ujenzi wa jengo la ghorofa. Pia namshukuru Mkurugenzi wa Jiji kuwa bega kwa bega, Vile vile nawashukuru walimu wote kwa kufanya kazi kwa bidii na ushirikiano.” Ameongeza Mwl. Gadi.

Mwalimu Gadi alitumia nafasi hiyo pia kumpongeza Mbunge wa Jimbo la Ilala Mussa Zungu na Diwani wa kata ya Upanga Mashariki Sultan Salimu katika kusimamia utekelezaji wa Ilani ya chama vizuri hasa sekta ya Elimu .

Awali akitoa mafunzo, Mwalimu wa Taaluma wa shule hiyo amesema ili kuleta ufanisi zaidi, utoaji wa elimu shuleni hapo ni shirikishi ambapo hushirikisha walimu wa Taaluma, wakuu wa idara, wakuu wa vitengo na wadhibiti ubora.