Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Korogwe
MFUKO wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Halmashauri ya Mji Korogwe mkoani Tanga imewataka wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa kuchangamkia fursa zilizopo kwenye nishati safi ya kupikia.
Moja ya fursa hizo ni kubuni miradi ya nishati safi ya kupikia ngazi ya kaya kama mkaa unaotokana na taka (Briquette), umeme unaotokana na samadi,kutengeneza majiko banifu yenye lengo la kupunguza matumizi ya mkaa ama kuni.
Hayo yamesemwa na Muwezeshaji wa TASAF Halmashauri ya Mji Korogwe Grace Kweka wakati anatoa warsha kwa walengwa wa TASAF, Mtaa wa Lwengera- Darajani iliyokwenda sambamba na malipo ya Septemba na Oktoba, 2024..
Kweka ametaja fursa nyingine ni kuwa mawakala wa kuuza mitungi ya gesi pamoja na majiko yake, walengwa kutumia nishati safi, ambapo itatoa fursa kwao ya kupata muda wa ziada wa kufanya shughuli za kiuchumi na kukuza kipato cha kaya.
“Kaya za walengwa kuwa na miradi ya upandaji wa miti ya matunda na mbao, ambayo itakuwa chanzo cha kipato cha kaya, wakati huo huo ikisaidia kusafisha hewa na kulinda mazingira. Walengwa wanaopata fursa ya kushiriki katika mafunzo ya stadi za msingi za kiuchumi, kuwa mstari wa mbele kubuni miradi inayochochea matumizi ya nishati safi ya kupikia.
“Walengwa kupeleka ujumbe kwa wanajamii wengine kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia, kwa maana ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wanajamii wengine, na walengwa kuhamasishwa kuandaa mipango ya uzalishaji inayohusiana na nishati safi ya kupikia kwa ajili ya ruzuku ya uzalishaji” alisema Kweka ambaye pia ni Ofisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Masuguru.
Akitoa somo kwa walengwa Mtaa wa Mahenge, Kata ya Kwamndolwa, Halmashauri ya Mji Korogwe, Afisa Ufuatiliaji wa TASAF (TMO) kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, na Halmashauri ya Mji Korogwe Elizabeth Mwantyala alisema vikundi vya kuweka na kuwekeza ni endelevu, na havitakiwi kuvunjwa, bali kama ni faida wagawane, lakini waendelee kuweka tena.
“Jamani, hivi vikundi ni endelevu. Wale wanakikundi napenda mkumbuke hili, inapofika mwisho wa mwaka mnagawana akiba au na sehemu ya akiba, lakini msivunje maana vikundi hivi havivunjwi bali vinaendelea, ili siku moja mfike mahali muwe na mamilioni badala ya kila mwaka kuanza na sifuri. Hivi vikundi vyetu ni kampuni, na siyo VICOBA ni vikundi vya kuweka na kuwekeza kwa ajili ya kukuza uchumi wa kaya”amesema Mwantyala.
Mratibu wa TASAF Halmashauri ya Mji Korogwe Rehema Letara alisema kwa malipo ya Septemba na Oktoba, 2024, jumla ya kaya ni 1,076, na malipo ya jumla ni sh. 33,466,000, ambapo malipo yaliyofanyika kwa njia ya mtandao ni sh. 23,206,000, na kaya zilizolipwa ni 743, huku malipo ya fedha taslimu ni sh. 10,260,000 kwa kaya 333.
More Stories
Bodaboda wamchangia Rais Samia Mil 1 ya fomu ya Urais
HAYA HAPA MATOKEO YOTE FORM II NA DARASA LA IV
Ufaulu waongezeka matokeo ya Darasa la Nne na Kidato cha Pili