January 30, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakuu wa nchi Serikali za Afrika waja na mikakati madhubuti ya uimarishwaji nishati



Na Penina Malundo,Timesmajira

KUPITISHWA na kusainiwa kwa azimio la Da es Salaam na Wakuu wa nchi na Serikali za Afrika katika mkutano wa Nishati wa Mission 300, Wakuu hao wameungana kwa pamoja na kuja na tatuzi ambazo zitaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza kasi ya usambazaji umeme barani Afrika na kuwaunganisha watu milioni 300 na umeme katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Marais mbalimbali waliohudhuria kutoka nchi ya Burundi, Botswana, Congo, Comoros, Djibouti, Ethiopia, Gabon, Ghana, Guinea Bissau, Kenya, Lesotho, Liberia, Libya, Madagascar, Malawi, Mauritania, Nigeria, Sierra Leone, Somalia na Zambia pamoja na kushuhudiwa na Wawakilishi wa Wakuu wa Nchi na Serikali, Wakuu wa Mashirika ya Fedha ya Kimataifa, Mashirika ya Kimataifa, Sekta Binafsi na Asasi za Kiraia wamekuja na tatuzi hizo baada ya kuona namna gani nchi za Afrika zilizokuwa zinakabiliwa na changamoto ya umeme na nishati ya kupikia katika kuleta maendeleo.

Kila nchi imeweza kuonesha uzoefu wake katika kutoa maoni yake namna zinavyokabiliana na changamoto ya nishati kupitia majadiliano huku zikitoa mkakati madhubuti wa kuhakikisha zinaendeleza agenda ya Mkutano wa nishati wa Wakuu wa nchi za Afrika Misheni 300.

Kupitia mijadala mbalimbali iliyowasilishwa na baadhi ya marais kutoka nchi za Afrika zinaonesha kwamba nchi za Afrika kwa sasa haziwezi kubaki gizani tena wala kuwa bara masikini bali linaelekea kukuza uchumi kupitia miundombinu ya kusafirisha umeme na kuwafikia wananchi wake.

Sasa ni wakati wa kuhakikisha Afrika inafunga gepu lililopo la umeme kwa asilimia 100 na kuona umuhimu wa kuzalisha umeme kwa kutumia kila tulichonacho ikiwemo maji,jua,upepo jotoardhi na gesi katika kuhakikisha umeme unawaka na kusukuma maendeleo.

Akizungumza katika Mkutano huo wa Wakuu wa Nchi,Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ni mwenyeji wa mkutano huo,anasema kuwa kwa kutoa kipaumbele katika upatikanaji wa nishati ya umeme, katika mkutano huo ulioandaliwa kwa ushirikiano na Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika utawezesha kuleta mageuzi ya kiuchumi, kukua kwa viwanda, kupunguza umaskini na kuimarisha ustawi wa watu.

Anasema mkutano huo umefanikiwa kupata ahadi za ufadhili wa Dola za Marekani Bilioni 40 kutoka Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa ajili ya kuwezesha usambazaji wa umeme barani Afrika.

Rais Samia anasema jumla ya nchi za Afrika 12 zimeingia kwenye Mipango Mahsusi wa Kitaifa kuhusu Nishati.''Kupitia Mpango Mahsusi kuhusu Nishati, Tanzania inakusudia kuvutia mitaji na uwekezaji zaidi itakayowezesha kuongeza uzalishaji wa umeme nchini na kukukamilisha kuunganisha Mtandao wa Umeme wa Tanzania na nchi jirani ili kuwezesha biashara ya kuuza na kununua nishati hiyo.

''Mpango huo utawezesha Serikali kukamilisha usambazaji umeme katika vitongoji vyote 64,359 nchini ifikapo 2030 na kupandisha kiwango cha uunganishaji wa umeme kutoka asilimia 46 ya sasa hadi kufikia asilimia 75,''anasema Rais Samia.

Rais Dkt. Samia amekuwa kinara wa matumizi ya nishati safi ya kupikia ameweka bayana kuwa mpango huo wa nishati pia utasaidia kuongeza upatikanaji wa nishati safi ya kupikia, ikiwemo gesi asilia na majiko banifu.

"Nchini Tanzania utegemezi wa kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia ni zaidi ya asilimia 90,hatuwezi kupuuza madhara na gharama kubwa ya kutumia kuni na mkaa hasa kwa afya na ustawi wa wanawake na wasichana.

"Katika kukabiliana na hilo Tanzania tumeweka mkakati wa kitaifa wa nishati safi ya kupikia unaolenga kupandisha kiwango cha matumizi ya nishati safi ya kupikia toka asilimia 10 ya sasa hadi asilimia 80 ifikapo 2034," anasema.


Anasema mpango huu utasaidia usambazaji wa Nishati safi ya kupikia kwani inakadiliwa takribani watu 950 barani Afrika wanakosa nishati hiyo safi ya kupikia hali ambayo inalighalimu bara hilo kwa kuhusishwa na kuongezeka kwa umasikini, vitishio vya kiafya, uharibifu wa mazingira,kuongezeka uzalishaji wa kaboni, kupotea kwa baonuai na kukosekana kwa usawa wa kijinsia.

Hakainde Hichilema Rais wa Zambia,ameipongeza nchi za Afrika kuingia katika mpango huo wa misioni 300 na kuipongeza Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika katika kuwaunganisha katika mpango huo.

Anasema nchi yake ni miongoni mwa nchi 12 zilizokubaliana na mpango huu ambapo wamekubaliana kuongeza uzalishaji wa umeme katika viwanda na matumizi ya majumbani.

"Zambia imedhamiria kwa dhati kufikisha umeme kwa watu wote kwani wanahitaji nishati ambayo ni nafuu ambayo watu wengi wataweza kuimudu na kupata unafuu wa nishati ya umeme kama uzalishaji utakapoongezeka.

"Kila nchi inaahadi zake na sisi pia tumehaidi na kusaini azimio la misheni 300,kwa kuona ni jambo la msingi ambalo watalifanya baada ya kutoka katika mkutano huu,sote tunazungumzia kuhusu nishati ila tunatambua changamoto za tabianchi na tunatambua hilo.

"Zambia miezi 24 iliyopita tulikuwa na ziada ya nishati ya umeme asilimia 84 na zambia ilikuwa ya kijani kabisa ,hatukuwahi kutarajia kwamba tungeweza kupata janga kubwa la ukame katika historia ya nchi yetu na janga hilo lilifanya kupoteza megawati mbili za uwezo wetu wa kuzalisha umeme,"anasema.

Aidha anasema awali walikuwa na kiwango kikubwa cha ziada ya umeme na kuuza umeme kwenye soko la umeme la kusini mwa Afrika lakini ndani ya muda mfupi waliweza kupoteza kabisa uwezo huo wa kuzalisha nishati hiyo.

Anasema hawakuweza kuzalisha nishati kwa matumizi ya kwenye kaya na viwanda vyao kupitia changamoto hiyo ila kupitia somo hilo na kutokuwa na vyanzo mbalimbali ya kuzalisha nishati ndio chanzo kilichowafikisha hapo.

"Mkutano huu wa Misheni 300,naamini baada ya kusikiliza mazungumzo mbalimbali hususan kipengele cha uwepo wa vyanzo muhimu vya umeme ili kuwa na uwezo na kuwa na umeme timilifu, ili janga linapotokea kama vile ukame wanaweza kulihimili,"anasema.

Anasema kama Zambia sasa wanapaswa kuwa na mchanganyiko wa vyanzo mbalimbali vya kuzalisha umeme na kuweza kuzalisha umeme na kuuza ulaya kwa kuptia nyaya za chini ya bahari,kuongeza uwezo wa kuzalisha umeme ambao utachanganywa na vyanzo mbalimbali.

Kwa upande wake Mfalme wa Lesotho,Letsie wa Tatu anasema mkutano huo ni ushahidi katika bara zima la afrika kushughulikia upatikanaji wa nishati endelevu kwa wote.

Anasema kuzindua kwa agenda 300,zimewafanya bainisha mikakati yao katika kutengeneza njia ya kuboresha maisha ya watu kupata umeme ambao utawaletea maendeleo.

"Nchi za Afrika ikiwemo Lesotho imebarikiwa kuwa na rasilimari nyingi na fursa nyingi,lakini bado zaidi ya watu milioni 600 ambao ni asilimia 80 ni sehemu ya upungufu wa nishati ya umeme.

"Umasikini wa nishati unazuia maendeleo ya kiuchumi na kupunguza fursa za elimu na huduma za afya,jitihada za lesotho kuelekea nishati kwa wote inaongozwa na ubunifu na ujumuishi na kutumia fursa za nishati jadidifu ambazo ni nyingi ikiwemo jua,upepo na maji ili kuweza kutafuta ufumbuzi wa kibunifu wa kinishati.

"Kwetu sisi kufikia malengo haya ya mageuzi ya misioni 300,tunalenga maeneo kadhaa muhimu kama kupanua nishati jadidifu kupitia mpango wetu wa kujenga mazingira muafaka kwaajili ya nishati safi ambayo itakidhi mahitaji ya majumbani na kuiweka lesotho kama msafirishaji wa nishati jadidifu,kuimarisha mtangamano wa kikanda kwa kuweka kipambaumbele wa kuuhisha mtandano na kuharakisha kupeleka umeme kwa ngazi ya chini ya vijijini," anasema.

Naye Rais wa Jamhuri ya Malawi,Dkt. Lazarus Chakwera anasema kama viongozi kupitia mkutano huo wa nishati lazima waje na tatuzi kwa kuhakikisha wanashughulikia jambo hilo la nishati kwa nchi za Afrika.

Anasema Malawi ni miongoni mwa nchi iliyoingia katika mpango wa kuhakikisha inapata nishati kupitia misheni 300 na kuhakikisha kwamba nishati hiyo inaweza kuwafikia watu wao wote na kwamba mikakati yao inauwiana na mision 300 hususan katika lengo la sita la mpango wa milenia wa maendeleo ya kimataifa.

Dkt, Chakwera anasema katika utawala wake malawi imeweza kuongeza uwezo wa uzalishaji wa nishati kutoka asilimia 12 kwa miaka minne iliyopita hadi kufikia asilimia 25 kwa sasa na wananchi wengi wa malawi kufikiwa na umeme.

"Kupitia misheni hii,tunatakiwa kuongeza kasi kutoka asilimia 25 hadi asilimia 70 kufika mwaka 2030,hivyo wanatarajia kuongeza uwezo wa kupata nishati jadidifu na kugusa nyumba milioni 2.7 kwa kupitia nishati katika ndani ya gridi na nje ya gridi ya taifa.

"Tutaweza kupata vizuri agenda ya viwanda na kutengeneza fursa za ajira kuharakisha ujasilimari kwa vijana na wanawake ambao ni uti wa mgogo wa uchumi wa nchi,''anasisitiza.

Hata hivyo Dkt.Akinumwi Adesina ambaye ni Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB),anasema upatikanaji wa umeme ni jambo la muhimu katika bara la Afrika na ukosefu wa nishati hiyo unadhohofisha uchumi wa nchi.

Anasema asilimia kubwa ya waafrika kwa sasa hawana umeme na ndio maana wameleta ajenda hiyo ya Mission 300 ili kuhakikisha watu wanafikiwa na huduma hiyo ili kukuza uchumi wa nchi za Afrika.

"Ili kuweza kufanikiwa katika hili ni vema kuunganisha mikono kwa pamoja katika kuhakikisha sekta ya umeme na nishati safi inafanikiwa kwa kiasi kikubwa.

"Hatutaweza kufanikiwa jambo hilo kama hatutaweza kufanya kazi pamoja na sekta binafsi na ndio maana nao wamefika katika mkutano huo kukubaliana ni kwa namna gani watatekeleza jambo hilo la kuwafikishia umeme watu ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kutengeneza ajira,"anasisitiza.

Anasema Benki ya Dunia (WB) na AfDB wanalenga kutoa Dola za Marekani Bilioni 40 kama kianzio cha kuhakiksha wanafanikiwa katika Mission 300.