December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakurugenzi, Maafisa Elimu Mkoa wa Tanga watakiwa kuweka mabango kwenye ofisi za serikali

Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online Tanga

Wakurugenzi na Maafisa Elimu katika Mkoa wa Tanga wametakiwa kuweka mabango kwenye ofisi za serikali yanayoelekeza “HUDUMIA MWALIMU KWANZA” ili walimu waweze kupata huduma kwa haraka na hatimaye warejee mashuleni kufundisha wimbi kubwa la wanafunzi waliowaacha madarasani.

Kauli hiyo imetolewa na Afisa elimu Taaluma Mkoa wa Tanga Onesmo Simime wakati wa kikao cha wadau wa elimu kilichoketi wilayani Muheza, kikao kilichoambatana na utoaji wa tuzo kwa shule zilizofanya vizuri, walimu na wanafunzi kama sehemu ya kuwapa motisha.

Afisa elimu huyo amesema kuwa ucheleweshwaji wa huduma kwa walimu pindi wanapokwenda kwenye ofisi za serikali ndio chanzo cha walimu kushindwa kufundisha kwa ufanisi jambo linalopelekea taaluma ya elimu kushuka kutokana na walimu kutumia muda mwingi katika foleni wanapofuata huduma mbalimbali.

“Mimi kama Ofisa elimu taaluma niwaombe viongozi wote ikiwemo wakurugenzi na maafisa elimu ikiwezekana waandike mabango kwenye ofisi ya mkurugenzi kwamba hudumia mwalimu kwanza ili mwalimu awahi akafundishe wale watoto 300 aliowaacha madarasani sio mwalimu anakuja anasota na foleni na ukishamsotesha akisharudi kule kazini ataishia tu kupiga stori kwamba ofisi haitujali hivyo hatofanya kazi kwa ufanisi, “alisistiza Simime.

Amesema iwapo jambo hilo litafanyiwa kazi itasaidia kwa kiwango kikubwa kupandisha hali ya ufaulu katika mkoa wa Tanga kutokana na walimu kutokuwa na vikwazo vinavyowapotezea muda ambapo lengo la kufanya hivyo itasaidia kuokoa vizazi vijavyo lakini pia Taifa litapata watu makini na wasomi.

Awali akifungua kikao hicho Mkuu wa wilaya ya Muheza Halima Bulembo hali ya ufaulu katika wilaya ya Muheza kwa sasa sio nzuri hivyo kupitia kikao hicho kilichowakutanisha wadau wa elimu kwa pamoja itasaidia kuinua kiwango cha elimu.

Bulembo amesema kuwa serikali ya Rais Samia imekuwa ikiboresha sekta ya elimu hivyo ni vyema walimu wakahakisha hawakwamishi juhudi hizo za Rais ambapo ameahidi kushirikiana nao bega kwa bega ili kuhakikisha wilaya hiyo inakuwa mfano wa kuigwa.

Pili Maximilian ni afisa elimu msingi wilaya ya Muheza amesema lengo la kikao hicho ni kuona hali halisi ya maendeleo ya elimu katika wilaya ya Muheza ambapo kwa ujumla katika ufaulu kwenye mitihani ya kitaifa ni ya wastani ambapo kwa shule za msingi darasa la saba ufaulu upo asilimia 78 na darasa la asilimia 97.

Pili alisema wamejiwekea mikakati ya kuhakikisha wilaya ya Muheza inafanya vizuri katika mitihani yake ya kitaifa wanashirikishana kwa pamoja ili kuweza kuinua kiwango cha elimu licha ya baadhi ya changamoto zilizopo.

Kati ya shule zinazofanya vizuri wilayani humo katika matokeo ya mitihani ya Taifa ni pamoja na shule ya Livingstone boys Seminary ambapo Mkuu wa shule hiyo Mchungaji Innocent Kamote amesema tangu waanzishe shule hiyo wamekuwa wakifanya vizuri ambapo wamekuwa wakishika nafasi ya kwanza kiwilaya na nafasi ya nne kimkoa ambapo lengo lao ni kuhakikisha wanashika nafasi ya kwanza kitaifa.

Mchungaji Kamote amezialika shule nyingine kwenda kujifunza shuleni hapo ili na zenyewe ziweze kufanya vizuri lengo likiwa ni kukuza taaluma ya elimu nchini.

“Tangu tulipoanza masuala ya kitaaluma tumekuwa tukifanya vizuri 2015 tulitoa form four yetu ya kwanza na tunaelekea kutoa form four yetu ya 8 na zote zimekuwa zikifanya vizuri tangu wakati huo tumekuwa tukishika nafasi ya kwanza hapa Muheza na nafasi ya nne kimkoa huku nafasi kadha wa kadha kitaifa siri kubwa ya shule yetu kufanya vizuri kwanza ni upendo kwa kuwa shule yetu ni dini, “alisema Mchungaji Innocent.

Mchungaji Kamote amesema kuwa kuna kanuni tano kubwa za kumfanya mwalimu kuwa mwalimu mzuri na kuwa na mafanikio katika taaluma ambapo jambo la kwanza ni upendo ambapo anapaswa kuwapenda wanafunzi wake, jambo la pili ni mwalimu kuwa na ujuzi wa anachokifundisha kwa kulijua vyema somo lake, jambo la tatu ni kujua kufundisha, jambo la nne kuwajua watoto wake, na jambo la tano ni kupenda kile ambacho anakifundisha.