November 15, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkurugenzi wa huduma za Uuguzi na Ukunga Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoro Bi. Ziada Sellah akisisitiza jambo wakati akifungua mafunzo wezeshi ya kujadili namna ya uboreshaji wa huduma za ukunga nchini,jijini Dodoma.

Wakunga wajizatiti kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi nchini

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online,Dodoma

WADAU wa Uuguzi na Ukunga wamekutana na kupanga mikakati ya kupunguza vifo vitokananvyo na uzazi na watoto wachanga kwa kuhakikisha huduma zinakuwa bora ikiwa ni Pamoja na kushirikisha walimu wa vyuo mbalimbali vinavyozalisha wanafunzi wa taaluma hiyo.

Mkurugenzi wa huduma za Uuguzi na Ukunga Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoro Ziada Sellah akisisitiza jambo wakati akifungua mafunzo wezeshi ya kujadili namna ya uboreshaji wa huduma za ukunga nchini,jijini Dodoma.

Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi wa huduma na Ukunga na Uuguzi kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ziada Sellah wakati akifungua semina fupi kwa niaba ya Mganga mkuu wa Serikali ambapo semina hiyo iliwashirikisha Wizara ya afya, Ofisi ya Rais-TAMISEMI,wakufunzi wa vyuo na Chama cha Wakunga Tanzania (TAMA) kwenye hospitali ya Benjamin Mkapa jijini hapa.

“Tumeangalia kwa upana wake na kuweka mikakati mbalimbali ya jinsi huduma zinazotolewa na wakunga kwa wajawazito ikiwa ni Pamoja na kuwapa mazingira wezeshi, huduma nzuri kwa wateja lakini pia tumewashirikisha walimu wa vyuo vya ukunga ili wafundishe somo la huduma kwa mteja ili isijekua ni kitu kipya kwa wanafunzi wanapoingia kazini” amesema Ziada.

Ziada amesema Wizara kupitia kurugenzi ya Uuguzi na ukunga itahakikisha wakunga wanapata mafunzo wakiwa maeneo yao ya kazi kupitia kwa wauguzi wakuu wa Wilaya na Mikoa pamoja na wauguzi viongozi ili kuweza kuboresha ukunga lengo likiwa ni kupunguza vifo vitokavyo na uzazi.

“Tumeangalia kwa upana kuanzia huduma zinapoanza kutolewa upande wa huduma ya Uzazi,Mama na Mtoto pale mama anapoanza kliniki na kuelekeza jinsi gani ya kutoa huduma ikiwemo vidokezo hatarishi kwa mama mjamzito pamoja na kutoa rufaa nmapema endapo kesi hawatoiweza,hivyo tutawajengea uwezo wakunga kwani asilimia 90 ya akina mama wote wanaojifungua wanahudumiwa na wakunga” amesisitiza Ziada.

Naye Rais wa Chama cha Wakunga Tanzania Chama cha Wakunga nchini (TAMA) Fedy Mwanga amesema chama kimejidhatiti kutoa elimu kwa wauguzi na wakunga nchini kuhusiana na huduma bora za uzazi kwa mama mjamzito kabla na baada ya kujifungua lengo likiwa ni kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.

Amesema chama hicho kinaandaa makongamano kwa ajili ya wakunga nchini ili waweze kupata elimu na kukumbushwa maadili katika utoaji wa huduma pale mama mjamzito anapofika katika sehemu ya kutolea huduma za afya.

“Leo tumeita wadau mbalimbali kwa ajili ya kuendeleza shughuli zetu za utetezi wa kuimarisha shughuli za ukunga Tanzania kwa kujua kabisa vifo vitokanavyo na uzazi nchini bado viko juu na vinazuilika, kwa kutambua umuhimu wa huduma za ukunga katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi tunakutana ili kukumbushana wajibu wetu katika kupunguza vifo hivyo” amesema Fedy.

Fedy amesema mkunga akiwa na stadi zinazostahili na akisimamiwa vizuri na kufanya kazi katika mazingira wezeshi anaweza kumuhudumia mama na kupunguza vifo kwa asilimia 87 hivyo chama cha wakunga nchini kina wajibu wa kufanya vikao na wadau ili kuweza kujadili namna wanavyoweza kufanikisha mazingira wezeshi kwa wakunga nchini.

Wakati huo huo Msimamizi wa huduma za Uuguzi na Ukunga kutoka OR-TAMISEMI Dinna Atinda amesema wataendelea kuboresha na kusimamia huduma za uuguzi na ukunga kwenye halmashauri zote nchini ili watoa huduma ngazi zote wanapata mafunzo na usimamizi mzuri ili kuendelea kutoa huduma nzuri na kwa uweledi kwa wananchi na kuweza kupunguza vifo vitokananvyo na uzazi.

Katika kukabiliana na changamoto za watumishi amesema serikali inaendelea kutoa ajira kila mwaka kwa watumishi wenye sifa na weledi ili kuweza kupunguza vifo vitokananvyo na uzazi na watoto wachanga.