November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakumbuka Septemba 11 ya simanzi

WASHINGTON, Rais Joe Biden wa Marekani amesema umoja wa kitaifa ndiyo nguvu kubwa ya Marekani katika nyanja mbalimbali.

Hayo ameyasema katika ujumbe wake wa kumbukumbu ya miaka 20, tangu mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11, yaliyoua watu 3,000.

Katika hotuba iliyotumwa mitandaoni, Rais Biden amesema pamoja na hisia kali za umoja wa kitaifa, baada ya tarehe 11 Septemba 2001, Marekani imeshuhudia pia ushujaa kila mahali, hata maeneo ambayo hayatarajiwi.

Aidha, Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Jen Psaki, amesema leo Rais Biden na mkewe, watakwenda kutoa heshima zao, kwa wahanga wa mashambulizi hayo, katika maeneo matatu yalikofanyika ambako ni New York City, Penn-Sylvania, na Pentagon.

Mashambulizi hayo ya kigaidi kwa kutumia ndege za abiria, ndiyo pekee yaliyowahi kufanywa na maadui wa kigeni ndani ya ardhi ya Marekani, katika historia ya taifa hilo lenye nguvu kubwa za kijeshi Duniani na iliyatumia kama sababu ya kuvamia Afghanistan na Iraq.

Wakati huo huo, Malkia Elizabeth wa Uingereza amesema, anaendelea kuwakumbuka na kuwombea waliopoteza maisha na manusura wa mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11 yaliyofanyika nchini Marekani mwaka 2001.

Pia amepongeza ushirikiano wa jamii katika kuijenga upya Marekani baada ya tukio hilo la kushtua ambalo lilileta zimanzi katika maeneo mengi duniani.

Katika Ujumbe aliomtumia Rais Joe Biden kwenye kumbukumbu ya miaka 20 ya mashambulizi hayo, Malkia amesema anaendelea kuliombea taifa la Marekani na familia zilizoathirika pamoja na wafanyakazi wa dharura waliokuwa kazini siku hiyo.

Wakati huo huo, Rais wa Korea Kusini, Moon Jae-in pia ametoa salamu zake za kumfariji rais wa Marekani Joe Biden na watu wa Marekani katika kumbukumbu hiyo ya miaka 20 tangu kutokea kwa mashambulizi hayo.

Rais Moon amesema, Korea Kusini kama mshirika muhimu wa Marekani itaendelea kusimama pamoja na taifa hilo katika vita vyake dhidi ya ugaidi duniani.