September 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakulima watakiwa kutumia maonesho ya nanenane kujifunza mbinu za uzalishaji karanga

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

KAMAPUNI ya Alssem inayojishughulisha na uzalishaji wa mbegu za karanga imetoa wito kwa wakulima nchini  kutumia maonesho ya Nanenane kujifunza mbinu za uzalishaji wa zao la karanga kwa kuzingatia kanuni bora ikiwemo kutumia mbegu zenye ukizani ili kuendeleza zao hilo kwa manufaa ya kibiashara.

Hayo yameelezwa jijini hapa ,leo Agosti 2,2024 na Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo Dkt.Emmanuel Monyo wakatu akizungumza na na waandishi wa habari katika banda lao lililopo kwenye viwanja vya Nanenane Dodoma na kusisitiza wakulima kupanda mapema mbegu za zao hilo kwa kuzingatia kupanda katika nafasi zilizopendekezwa bila kusahau kupalilia kwa wakati ili kupata mazao mengi na Bora kuendana ulimwengu wa kidigitali.

“Mkulima ili aone tija ya kilimo chake ahakikishe anakausha mavuno mara baada ya kuvuna na Kuhifadhi mahali pasipo na unyevu ili mbegu yake isiharibike,”amesema.

Aidha Dkt.Monyo ameeleza umuhimu wa karanga kuwa ni zao hilo ambalo amelitaha kuwa na faida nyingi ikiwemo kuzalisha mafuta ambayo hutumika kama chakula cha binadamu huku mashudu na majani yake kutumika kulisha mifugo.

Kwa upande wake Emmaculate Chaula ambaye ni mdau wa kilimo cha Karanga ametaja aina za karanga ambazo mkulima anapaswa kuzitumia kutokana na ubora wake kuwa ni Naliendela ambayo hukomaa kwa siku 90 Hadi 100 na mkulima akilima kutegemea kupata mavuno ya wastani wa tani 1 kwa hekta.

Aina nyingine ni Ndachi ambayo kukomaa kwa siku 110 na mkulima akilima kupata mavuno wastani wa tani 1.1-2 kwa hekta huku akiitaja mbegu ya Nari nut kustawi katika Ukanda wa chini na Kati na kukomaa kwa wastani siku 106 hadi 110 na inatoa mavuno ya wastani wa tani 1.3 hadi 2 kwa hekta.

“Nyingine ni Tanzanut,hii inastawi katika ukanda wa miracle 0 hadi 1500 kutoka usawa wa habari na inakomaa kwa wastani wa siku 116 na inatoa mavuno ya wastani wa tani 1.5 kwa hekta, wakulima wanapaswa Kuzingatia mbegu hizi ili kulima kilimo chenye faida, ” amesisitiza