December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakulima wafurahia mikopo zana za kilimo


Na Joyce Kasiki,Dodoma

MKUU wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule ameipongeza kampuni ya PASS LEASING kwa kuona umuhimu wa  kuwadhamini wakulima mikopo ya vifaa  vya kilimo vitakavyowawezesha kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao.

Akizungumza katika maonesho ya wakulima na wafugaji viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma mara baada ya kukabidhi vifaa hivyo ambavyo ni matrekta,magari makubwa ya kubebea mazao shambani na mashine rahisi za kuchakata mazao kwa udhamini wa PASS LEASING ,Senyamule amesema,kufanya hivyo ni kuunga mkono kurudi za Rais Samia Suluhu Hassan za kuleta maendeleo ya wananchi nchini.
“Naipongeza PASS LEASING kwa kuunga mkono juhudi za Rais Samia kwa kuwekeza kwa wakulima hawa ambao sasa naamini wanakwenda kuongeza tija katika uzalishaji wao,

“Maana wametoka sasa kwenye matumizi ya jembe la mkono na kutumia nguvu  na badala yake wanaenda kwenye matumizi ya Teknolojia ambayo inakwenda kuwakomboa kiuchumi.

Awali  mnufaika wa vifaa hivyo  Minza Mlela  ameishukuru kampuni ya PASS LEASING kwa kumkubadhi Trekta ambayo itaenda kufanya Mapinduzi makubwa kwenye sekta ya kilimo na hivyo kumuongezea tija katika kilimo.

“Kabla ya kupata trekta hili nilikuwa nalima kwa kutumia jembe la mkono , heka 200 nilikuwa natumia muda mrefu ,lakini sasa hivi nitalima kwa muda mfupi lakini na wakulima wengine watalima kupitia trekta langu.”amesema

Awichi Njarika mkazi wa Pandambili wilaya ya Kongwa mkoa wa Dodoma ambaye pia ni mnufaika amesema  huko nyuma alikuwa analima kwa  kutumia jembe la mkono  .

Amewaasa  wakulima wenzake waachane na kilimo cha kizamani kwa sababu kuna fursa za mikopo kwenye taasisi mbalimbali hasa zinazojihusisha na masuala ya kilimo.