Na Allan Kitwe,Timesmajiraonline,Tabora
WAKULIMA na wafugaji wa Mikoa ya Tabora na Kigoma wametakiwa kwenda na kasi ya mabadiliko ya teknolojia na kuzingatia maelekezo ya wataalamu ili kuongeza uzalishaji wa mazao na mifugo na kujikwamua kiuchumi.
Ushauri huo umetolewa hivi karibuni na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma IGP Mstaafu Simon Sirro alipokuwa akiongea na viongozi na wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo na ufugaji katika viwanja vya nane nane, Ipuli Mjini Tabora.

Amesema kuwa ni muhimu sana kwa wakulima na wafugaji kuiga mambo mazuri yanayoweza kuleta mabadiliko chanya katika shughuli zao na kuwapeleka kwenye kiwango kingine cha uzalishaji.
Amefafanua kuwa ili kupata mafanikio makubwa, wakulima hawana budi kutumia zana bora na mbegu bora zinazozalishwa na Taasisi za Utafiti wa Kilimo zilizopo hapa nchini na kuzingatia kanuni zote za kilimo bora.
Aidha amesisitiza umuhimu wa kufuga kisasa na kuachana na ufugaji wa kizamani wa kuhama hama kwa kuwa hauna tija na unawaletea umaskini licha ya kuwa mifugo ni utajiri.
‘Wakulima na wafugaji nendeni ya kasi ya mabadiliko ya teknolojia, tumieni maonesho ya nane nane kuchota ujuzi na maarifa mapya ambayo yatawasaidia kupiga hatua kubwa zaidi katika shughuli zenu’, ameeleza.
RC Siro ameongeza kuwa kampeni ya chanjo na utambuzi wa mifugo iliyozinduliwa hivi karibuni na serikali ni nyenzo muhimu sana kwa wafugaji wote na zoezi hili linapaswa kuwa endelevu kwa ustawi wa mifugo yao.
‘Tumieni ipasavyo Vituo vya Utafiti wa Mazao ya Kilimo na Mifugo vilivyopo katika Mikoa hii ili kilimo na ufugaji wenu uwe wa kisasa na wenye tija katika uchumi wenu ikiwemo kuongeza mapato ya halmahauri na serikali, amesema..
Ametoa wito kwa Maafisa Ugani na Mifugo wa halmahauri zote kutokaa maofisini bali watembelee wakulima na wafugaji ili kuwapa elimu, mbinu na kanuni za kilimo na ufugaji bora utakaoleta mabadiliko katika shughuli zao.



More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako