Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online, Mbeya
WAKULIMA wa parachichi Halmashauri ya Mji Njombe mkoani Njombe wameiomba Serikali kuwapatia mikopo ili waweze kulima kilimo cha parachichi chenye tija zaidi
Pamoja na mikopo, pia wameomba kujengewa miundombinu ya maji kwa kuchimbiwa visima virefu, pampu za kuvuta maji na mabomba ya maji ili yafike kwenye mashamba yao, kwani kilimo hicho kinategemea maji kwa ajili ya umwagiliaji kwa zaidi ya asilimia 90.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Agosti 3, 2022, mmoja wa wakulima wa zao la parachichi kutoka Halmashauri ya Mji Njombe Stephen Mlimbila maarufu kama Nemes, alisema ipo haja ya vijana kupewa mikopo ili kuwekeza kwenye kilimo hicho.
“Tunaiomba Serikali kutoa mikopo kwa wakulima na hasa vijana ili waweze kushiriki kwa kikamilifu kwenye kilimo cha parachichi. Pia kilio kikubwa kwa sisi wakulima wa parachichi ni miundombinu ya maji. Tunaomba Serikali itusaidie fedha ituchimbe visima virefu, pampu za kuvuta maji na miundombinu ya mabomba ya maji kwenye mashamba yetu” alisema Mlimbila.
Mlimbila ambaye ana shamba la parachichi likifahamika kama Nemes Green Farm, na Halmashauri ya Mji Njombe imempeleka kwenye Maonesha ya Nane Nane Kitaifa mkoani Mbeya kama mkulima wa mfano, alianza kilimo hicho mwaka 2009 akiwa ameanza na miti tisa, na sasa ana miti ya parachichi 7,000 kwenye ukubwa wa ekari 120.
“Nimeanza kilimo cha parachichi mwaka 2009 nikiwa na miti tisa, na sasa nina miti 7,000 ya miparachichi. Nimeanza kuvuna mwaka 2013, na kila mwaka nafuna parachichi zaidi ya tani 100, na kilo moja ni kati ya sh. 1,500 hadi 2,000, itategemea na nguvu ya soko kwa wakati huo.
“Soko la parachichi zangu lipo India na Dubai, na halina shida sababu parachichi zangu zinatumia mbolea ya asili (samadi). Nia yangu ni kufikisha ekari 150, na hiyo inawezekana sababu shamba langu lipo kwenye hatua tofauti ya zao la parachichi, kuanzia miche iliyopandwa na miti inayovunwa” alisema Mlimbila.
Ofisa Kilimo wa Halmashauri ya Mji Njombe Henry Kideula amesema idara yake inatoa mikopo kwa wakulima kupitia Mfuko wa Taifa wa Pembejeo (AGITF), hivyo wakulima wa parachichi na mazao mengine wajitokeze kuomba mikopo hiyo.
“Ipo mikopo kwa ajili ya kufungiwa mifumo ya umwagiliaji maji, uchimbaji wa visima virefu, trekta na vyombo vya kusaidia kuvuna mazao” alisema Kideula.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa