Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Tanga
WAKULIMA wa Wilaya ya Handeni mkoani Tanga wataondokana na adha ya kusafirisha mazao yao kwenye barabara mbovu baada ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kuwa na mpango wa kujenga barabara kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita 147.
Barabara hizo ni Mkata- Kwasunga kilomita 21.85, Sindeni- Kwedikwazu kilomita 37.7, Michungwani- Kwadoya kilomita 21.85, Kwachaga- Kwankonje kilomita 10, Mzundu- Kabuku kilomita 17.6, na barabara ya Mkata- Kwamsisi ambayo ipo chini ya Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) itakuwa ya kilomita 38.
Hayo yalisemwa na Meneja wa TARURA Mkoa wa Tanga Mhandisi George Tarimo kwenye Kongamano la Uwekezaji, Biashara na Utalii sambamba na uzinduzi wa Mwongozo wa Uwekezaji wa Mkoa wa Tanga, huku kauli mbiu ikiwa ni ‘Wekeza Tanga kwa uwekezaji endelevu’ lililofanyika jijini Tanga kwa siku mbili, Novemba 16- 17, 2023.
Mhandisi Tarimo amesema ujenzi wa barabara hizo kwa kiwango cha lami upo kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji huku utaanza rasmi mwaka wa fedha 2024/2025.
“Ili kuboresha barabara za wananchi kwenye vijiji vya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, TARURA itajenga barabara kwa kiwango cha lami kwa urefu wa kilomita 147,” amesema Mhandisi Tarimo.
Mhandisi Tarimo amesema kwa mwaka wa fedha 2023/2024, watafanya matengezo ya aina mbalimbali kwenye barabara za halmashauri sita za Mkoa wa Tanga, ambapo kwa Halmashauri ya Mji Korogwe, watajenga daraja la mawe kati ya Mtaa wa Msambiazi na Kijiji cha Kwamasimba na Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe itajenga daraja la mawe kwenye barabara ya Makuyuni- Zege- Mpakani.
Halmashauri ya Bumbuli katika barabara ya Kibaoni- Kwanguruwe na Malumbi watajenga daraja la zege, Wilaya ya Pangani watajenga tuta na kuweka changarawe na makalavati barabara ya Bweni- Kikokwe- Mwera, na Wilaya ya Mkinga kwenye barabara ya Duga- Mwakijembe- Mgambo, watajenga tuta la barabara, kuweka changarawe na boksi kalavati mbili.
“Wilaya ya Kilindi kwa barabara ya Muungano-Kimembe- Tamota- Vyadigwa, tutajengwa tuta la barabara, kuweka changarawe, boksi karavati na daraja la mfuto (drift) na Wilaya ya Muheza kwenye barabara ya Kilulu- Mtindiro- Kwafungo kutajengwa daraja la mawe na kuweka changarawe kwenye barabara hiyo,” amesema Mhandisi Tarimo.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakaniÂ
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best