January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakulima, Maofisa Ugani wapewa darasa

Na Dotto Mwaibale, TimesMajira Online, Morogoro

TAASISI ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), kupitia Kituo chake cha Naliendele Mtwara, kimewataka wakulima wote wa zao la korosho kubadilika na kuanza kulima kilimo cha biashara kwa kuzingatia ‘agronomia’ stahiki, ili kuongeza tija na ubora wa zao hilo.

Mbali na hivyo, pia kituo hicho kimetoa angalizo kwa wakulima na wadau wa korosho kuhakikisha wanaepuka udanganyifu wowote wanapohitaji huduma ya mbegu bora ya zao hilo, badala yake wawasiliane na Maofisa Kilimo wa eneo husika ili kupata maelezo ya namna ya upatikanaji wake.

Mratibu wa zao hilo kitaifa kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo Tari Naliendele, Dkt. Geradina Mzena ameyasema hayo katika Mji Mdogo wa Gairo jwakati akifungua mafunzo ya kilimo bora cha zao la korosho kwa Maofisa Ugani na wakulima kutoka Halmashauri saba za Mkoa wa Morogoro.

“Tari Naliendele hatuuzi mbegu kwa fedha taslimu, lazima uwe na namba ya malipo na endapo ukiuziwa mbegu na mtu yeyote kwa fedha taslimu ujue umeibiwa. Korosho ni zao la kudumu, lina mfumo wake na kamwe usijaribu kupanda mbegu usiyoijua,” amesema.

Amesema, mbegu bora ya zao hilo na aina zake, huzalishwa na Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Tari Naliendele pekee na si kwingineko, hivyo wakulima wanapaswa kuwa makini ili kwa pamoja kuweza kuinua ubora wa zao hilo na kujihakikishia uwepo wa soko lake kitaifa na kimataifa.

Mtafiti huyo na Mgunduzi wa zao hilo, Dkt. Mzena amesema ili kubaini kama mbegu ya korosho husika ina ubora ni sharti idadi ya punje za korosho ziwe chini ya 200 kwa kilo moja na si zaidi ya hapo.

Alifafanua kwamba kilo moja ya zao hilo, inaposheheni punje zaidi ya 200 hudhihirisha wazi kuwa ubora wa mbegu hiyo, una mashaka na mkulima husika anapaswa kufika Tari Naliendele, ili kupatiwa mbegu mbadala zenye ubora.

Akizungumza mbele ya wakulima na Maofisa Ugani, Dkt. Mzena amesema korosho ambayo hulimwa na takribani Watanzania 283,000 nchini, ina faida kubwa katika kuongeza kipato cha kaya na kuondoa umaskini.

Amesema, Mtanzania yeyote atakayelima korosho ndani ya mikoa rafiki takribani 17 inayostawisha zao hilo ni dhahiri atajipatia fedha za kutosha kutokana na ukweli kwamba zao hilo, lina nguvu na utajiri mkubwa, tofauti na mazao mengine. Kikubwa ni kuzingatia kanuni bora za kilimo.

Naye Mtafiti Mwandamizi na Mdhibiti wa visumbufu vya wadudu na magonjwa kwenye zao hilo, Dkt. Wilson Nene amesema kituo hicho kinatoa mafunzo hayo lengo ni kuwawezesha wakulima na Maofisa Ugani, kuwatambua wadudu waharibifu, magonjwa na namna ya kukabiliana nayo ili kufikia shabaha tarajiwa kutoka tani 300,000 zinazozalishwa kwa sasa kufikia tani milioni moja ifikapo 2023.

Kituo cha Tari Naliendele, kimepewa majukumu ya kitaifa ya kutafiti, kustawisha na kuongeza tija na thamani kwenye mazao ya korosho na mbegu jamii ya mafuta, ikiwemo ufuta, karanga na alizeti.