March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakili Kilenzi:Wananchi jitokezeni  kupiga kura badala ya kuandamana

*Asisitiza watumishi kusimamia miradi kwa tija kuondoa chuki dhidi ya Serikali 

*Asisitiza Serikali kuongeza ukali wa kusimamia sheria kwa watumishi wazembe

Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza 

Jamii imehimizwa kushiriki katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 29,2025  ili kupaza sauti zao kupitia sanduku la kura bila kufanya maandamano ambayo madhara yake ni makubwa.

Huku Watumishi na watendaji wanaopata dhamana ya kusimamia miradi ya Serikali, kuhakikisha wanazingatia maadili ya utumishi wa umma  na kusimamia kwa tija miradi hiyo ili wananchi waweze kupata huduma bila malalamiko.

Wito huo umetolewa na Oktoba  3,2025, na Wakili Willbard Kilenzi,wakati akizungumza na vyombo vya habari ofisini kwake jijini Mwanza kwa ajili ya kusisitiza suala la kulinda usalama wa nchi si la Serikali wala polisi na vyombo vya dola pekee bali ni la kila mwananchi.

Ambapo amewaomba wananchi badala ya kufikiria maandamano  waendelee kusikiliza kwa makini kampeni za vyama vyote  na kuchagua ilani zao ili Oktoba 29,2025,wajitokeze kwa wingi  kupiga kura ili kupata Serikali inayotokana  na matakwa ya wananchi walio wengi.

Amesema na huo  ndio msingi  wa demokrasia  na ili uchaguzi umalizike kwa amani na salama kisha mambo ya mabadiliko(reform),yatazungumzika na kufanyiwa kazi.

“Kutokana na uzoefu wa maandamano tuliyoshuhudia kwenye nchi jirani za wenzetu madhara yake ni makubwa ikiwemo uharibifu wa miundombinu na mali za raia kwani wenye nia ovu pia wanaweza kutumia fursa hiyo kufanya uhalifu wa kupora mali na wizi,vifo ambavyo usababisha watoto kubaki yatima,wajane na wagane pamoja na majeruhi,”amesema Kilenzi.

Kilenzi,amesema,katika nchi zote za kidemokrasia matokeo ya kura uamua ni chama kipi kiunde Serikali ambacho kitashinda kwenye uchaguzi,hivyo amewahimiza wanaohamasisha maandamano kutumia nguvu hizo kuwashawishi watu kujitokeza siku ya uchaguzi kupigia viongozi wanaowaamini kuwa wataleta mabadiliko badala ya kuandamana.

Sanjari na hayo,Kilenzi amesema miradi ya maendeleo ambayo Serikali inawekeza fedha nyingi inapo suasua kufanya kazi inachochea wananchi kuwa na chuki na Serikali na wakati mwingine kutishia maandamano.

Hivyo amewahimiza watendaji waliopatiwa dhamana na Serikali ya kusimamia miradi ya maendeleo kusimamia kwa tija miradi hiyo kwani Rais hawezi kufika kila mahali.

“Maandiko yanasema mwanamke mpumbavu ubomoa nyumba yake kwa mikono yake mwenyewe.Na mimi nasema na raia mpumbavu anabomoa nchi yake kwa mikono yake mwenyewe,maana yangu ni kwamba  watanzania hawa hawa ambao tumepewa dhamana ya kusimamia mali za umma ndio tunafanya hivi na kusababisha nchi kuingia katika mfarakano,”.

Huku akiishauri Serikali kuhakikisha ina ongeza ukali wa kusimamia Sheria ili watumishi ambao hawawezi kusimamia miradi na kufanya kwa ushindani ili  faida  ipatikane na wananchi kunufaika, wachukuliwe hatua za kinidhamu na kisheria inapobidi.