November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakazi wa Tinde waishukuru Serikali

Na Suleiman Abeid,Timesmajira Online, Shinyanga

WAKAZI wa vijiji vya Jomu na Nyambui Kata ya Tinde Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga wameishukuru Serikali kwa hatua yake ya kuwapatia huduma ya maji safi na salama baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria.

Pia wananchi hao wametoa pongezi zao kwa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Manispaa ya Shinyanga (SHUWASA) ambao ndiyo wametekeleza mradi huo ndani ya muda uliopangwa hali ambayo imewezesha wananchi hao kuondokana na changamoto ya ukosefu wa maji.

Bomba kubwa linalotoa maji kwenye tanki lililopo Buchama kupeleka kwa wakazi wa Kata ya Tinde ambao wameanza kupata huduma ya majisafi na salama.

Monica Destory na Alexander Masebu wakazi wa Kata ya Tinde wamesema kukamilika kwa mradi huo kumewaondolea kero ya zaidi ya miaka 30 ya kutembea umbali mrefu kwa ajili ya kutafuta maji safi kwa ajili ya matumizi yao ya kila siku ambayo hata hivyo hayakuwa salama.

Wamesema wakazi wa Kata hiyo walikuwa wakifuata maji eneo moja tu linaloitwa Mwakisu kwenye mto Manonga na kwamba kutokana na eneo kuwa moja palikuwa na msongamano mkubwa na wengi iliwachukua muda mrefu kuyapata maji hayo na kujikuta kazi nyingine za kimaendeleo zikikwama.

“Mimi nina miaka zaidi ya miaka 30 hapa Kata ya Tinde, hali ya upatikanaji maji ilikuwa ni shida, tulikuwa tunayafuata kule mto Manonga, kutoka hapa ni umbali wa kilometa nne, kwenda na kurudi kilometa nane, tulitumia baiskeli, matela ya kukokotwa na ng’ombe, tulihangaika sana,”ameeleza Monica Destory na kuongeza kuwa

“Mara nyingi tulikuwa tunakesha huko, na hata wale waliokuwa wakifuata kwa ajili ya kuuza, tulikuwa tunauziwa dumu moja shilingi 500, lakini kwa sasa tunashukuru, changamoto hii imetuondokea, na kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo ya maji kichwani, imetimia,”.

Katika taarifa yake kwa waandishi wa habari waliotembelea mradi huo Kaimu Mkurugenzi wa SHUWASA, Sarah Emmanuel amesema mradi wa maji wa Tinde umegharimu kiasi cha bilioni 5.22 na utekelezaji wake ulianza mnamo Agosti 21, 2021 ukiwa umesanifiwa kuhudumia zaidi ya wananchi 60,000 kutoka katika vijiji 22.

Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Mazingira Manispaa ya Shinyanga (SHUWASA) Sarah Emmanuel (wa tatu kutoka kushoto) akitoa taarifa ya Mradi wa Maji Tinde kwa waandishi wa habari w mjini Shinyanga.

Sarah amesema miongoni mwa kazi ambazo zimefanyika katika utekelezaji wa mradi huo ni pamoja na ulazaji wa bomba kuu kutoka kwenye (Tapping Point) eneo la Didia hadi Buchama, bomba zenye kipenyo cha milimita 400, 250 na 150 na jumla ya urefu wa kilometa 16.

“Itakumbukwa ujenzi wa mradi huu ni muendelezo wa ujenzi wa mradi wa Tinde kwenda Shelui uliotekelezwa na Wizara ya Maji kupitia Mkandarasi M/S Megha Engineering and Infrastructure Ltd kwa gharama ya bilioni 24.47,”.

Ambapo ameeleza kuwa fedha hizo ni chenchi kutoka fedha zilizopangwa kutekeleza mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda katika Miji ya Nzega, Tabora na Igunga ambapo kwa sehemu ya Tinde pekee umegharimu bilioni 5.22 na wanaatarajia wananchi wapatao 60,000 katika vijiji 22 watanufaika na mradi huo.

Waandishi wa habari wakipata maelezo kutoka kwa mmoja wa watumishi wa SHUWASA kwenye tanki lenye ujazo wa lita 1,150,000 ambalo linasambaza maji kwa wakazi wa vijiji vilivyopo kwenye kata ya Tinde Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.

Mbali ya mradi wa Tinde, Sarah amesema pia SHUWASA inatekeleza mradi mwingine mkubwa katika Kata ya Didia Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga ambapo kiasi cha zaidi ya milioni 90,zimetenga na Wizara ya Maji kupitia mfuko wa maji.

Amesema fedha zitatekeleza ujenzi wa tanki la kuhifadhia maji lenye ujazo wa mita za ujazo 100 eneo la Didia ambapo tayari kiasi cha milioni 36 tayari kimepokelewa na SHUWASA ambapo mradi unatekelezwa na Mkandarasi M/S SBS Tanks Solution East Africa Ltd na unasimamiwa na SHUWASA ukiwa hadi sasa umekamilika kwa asilimia 99.

“Mradi huu umekamilika kwa asilimia 99 na umehusisha ujenzi wa msingi wa tanki, ufungaji wa column eneo la kazi, kufunga tanki na ufungaji wa panel za tanki na tayari mradi upo katika hatua za majaribio,” ameeleza Sarah.

Pamoja na mafanikio ambayo yamepatikana katika utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa ama kusimamiwa na SHUWASA, Sarah amesema bado zipo changamoto kadhaa zinazoikabili Mamlaka yake ikiwemo kutokufika kwa mtandao wa maji safi kwa baadhi ya wakazi waliopo pembezoni ya Manispaa.

Tanki la maji lenye ujazo wa lita 100 ambalo limejengwa katika kata ya Didia kwa ajili ya kusambaza maji kwenye vijiji vilivyopo kata ya Didia.

Hata hivyo amesema kwa mwaka 2023/2024 wamejiwekea mikakati itakayosaidia kukabiliana na changamoto zilizopo kwa hivi sasa ikiwemo kutoa huduma ya uhakika ya maji safi kwa wateja wake wa Manispaa ya Shinyanga.

Maeneo mengine yanayotarajiwa kupatiwa huduma hiyo ya maji safi mbali ya Manispaa ya Shinyanga ni miji midogo ya Tinde, Didia na Iselamagazi ikiwemo kuendelea kutumia uwezo wa ndani wa Mamlaka ili kupanua mtandao wa maji safi hatua kwa hatua kufikia asilimia 95 kwa mijini na vijijini asilimia 85 ifikapo 2025.