Na Martha Fatael, Moshi
UKATILI kwa siku za hivi karibuni umekuwa ajenda kubwa ikiongelewa zaidi ukatili wa kingono ambao umeshika kasi na unahitaji nguvu kubwa katika kuutokomeza tofauti na hali ya hapo nyuma ambapo ukatili uliongelewa zaidi kwa wanawake.
Ukatili kwa watoto pamoja na jitihada kubwa zinazofanyika, unaendelea kukua na matukio yanayoripotiwa yakiendelea kuchukua sura tofauti tofauti.
Ni katika hali hiyo, Mwandishi wa makala hii amejaribu kufanya utafiti kuhusu chanzo cha ongezeko hilo, ambapo baadhi ya wakazi wa kata ya Mabogini wilayani Moshi wananza kwa kuitaja sera na sheria.
Nuru Mustapha, Mwanaidi Juma na Abdala Sabuni, wanataja baadhi ya sababu za kuongezeka kwa matukio hayo ni pamoja na kutochukuliwa hatua kwa baadhi ya watuhumiwa kwa wakati.
Wanasema kumekuwa na uwepo wa udhaifu kwenye mifumo ya haki na kisheria hususani upungufu wa raslimali au kutokamilika, jambo ambalo linazuia uchunguzi kutofanyika kwa haraka na utekelezaji wa sheria.
“Hatuna kituo cha polisi karibu hili linaweza kuwa sababu ya ukatili kuendelea kwenye eneo letu maana aliyefanya tukio anapata nafasi ya kuharibu ushahidi ama kutoroka lakini pia wanaomsaidia mtoto kukata tamaa sababu ya gharama za kufikia haki” anasema Mustapha
Anasema ukiacha ukiacha sababu nyingine baadhi ya waathiriwa wa matukio hayo wanachagua kunyamaza kwa hofu ya kupata aibu Zaidi ama wanakumbwa na uoga wa hofu ya kulipizwa kisasi au kutoaminika na jamii ama vyombo vya sheria.
“Inakuta mtoto kabakwa ama kalawitiwa na baba wa kambo mama anakuwa upande wa yule baba…….hamwamini mtoto wake anaanza kumpiga na kumtishia kuwa acha kumsingizia baba yako….usiseme popote na bado mtu huyo anaendelea kuishi na mtoto huyo eneo hilo hilo”anasema Sabuni.
Sabuni anasema matukio haya yamekuwa yakiishia njiani kutokana na sababu moja wapo ya kukosa ushahidi wa kutosha, jamii inakataa kwenda kutoa ushahidi kwa hofu ya kukosana na mtuhumiwa ama ndugu zake, lakini pia wanahofia mtuhumiwa kuachiwa huru.
Makamu mwenyekiti wa kituo cha taarifa na maarifa kinachoratibiwa na Shirika la kutetea haki na kupinga ukatili wa kijinsia (TGNP) katika kata ya Mabogini,Bw. Hatangimana Justin anasema mtitiriko mrefu wa kufuata hadi kufikia haki kwa waathiriwa wa matukio ya ukatili ni miongoni mwa sababu ya matukio kuongezeka na kutofikia mwisho.
Anasema kwa elimu inayoendelea kutolewa imesaidia kuongezeka kwa matukio yanayoripotiwa lakini matukio mengi pia hayaripotiwi kwenye vyombo vya sheria kwa kuhofia kufuata mlolongo wa kiseria lakini umbali wa dawati la polisi pia.
“Nadhani kuna haja ya mchakato wa kisheria kwa waathiriwa wa matukio ya kikatili kutazamwa upya kwa kuondoa milolongo mirefu ili kuwarahisishia waathirika kukamilisha taratibu hizo lakini kuwapa urahisi wa kufuatilia”anasema.
Aidha anasema ni muhimu kwa vijana kushirikishwa kwa karibu kuhusu masuala yote ya ukatili na sheria zake ili kuwa sehemu ya kumaliza tatizo hilo ikiwa ni pamoja na hatua kuchukuliwa kwa haraka.
Kauli hii ya Mwenyekiti inaungwa mkono na Mbunge wa viti maalum mkoani Kilimanjaro, Ester Maleko ambaye anasema kwa kushirikiana na wabunge wenzake wataishauri serikali kufanya mabadiliko ya sera na sheria ili wanaume wawe sehemu yake.
Anasema kwa sasa sheria imefanyiwa marekebisho mara kadhaa ili kukabiliana na ukatili unaoendela lakini bado kwa kushirikiana na wabunge wenzake wataendelea kutoa mapendekezo mara kwa mara ili kuendana na mazingira yaliyopo.
Waziri wa maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake na makundi maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, kupitia hotuba yake kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2024/25 anasema mabadiliko ya sheria yameendela kufanyika ili kukabiliana na ukatili.
Anasema jumla ya matukio 799 ya ukatili dhidi ya watoto yameibuliwa na kuwasilishwa kwenye mamlaka za kusimamia sheria kwa hatua Zaidi kupitia makundi yanayokabiliana na ukatili lakini wasimamizi wa haki za watoto na wanawake.
Anasema pia hadi Aprili, 2024, jumla ya watoto 708,957 wanaoishi katika mazingira hatarishi wametambuliwa katika halmashauri zote nchini na kupatiwa huduma kuendana na mahitaji yao ikiwemo watoto 275,058 wamesaidiwa na serikali kwa kushirikiana na wadau kupata vyeti vya kuzaliwa. Aidha, Kaya za watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi 457,450 zimesaidiwa kupata Bima za afya.
Dkt. Ngwajima anasema hadi kufikia Aprili 2024, Jumla ya 51 watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi 284,308, wazee wasiojiweza 245 na waathirika wa matukio ya ukatili 2,682 (watoto 1,944 na watu wazima 738) wamepatiwa huduma ya msaada wa akili na kisaikolojia kutokana na kukabiliwa na changamoto mbalimbali za kimaisha katika jamii.
Aidha, anasema katika kipindi hicho huduma hii pia imetolewa kwa wahanga wa vitendo vya ukatili 13,926 (ke 7,142 na watoto 6,784) pamoja na wahanga wa vitendo vya ukatili wa usafirishaji haramu wa binadamu 452.
Hata hivyo waziri Gwajima anasema utekelezaji wa Mpango kazi wa taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto (MTAKUWWA) katika kupunguza au kumaliza ukatili ulizingatia takwimu za ukatili za ujumla zilizowasilishwa na Tanzania Demographic Health and Malaria Indicator Survey ya mwaka 2022, ambayo ilionesha kiasi cha ukatili wa kimwili kwa wanawake kuwa ni asilimia 40, na ukatili wa kingono kuwa ni asilimia 27, na ule unaotokana na ukeketaji kuwa ni asilimia 10.
Anasema kwa sasa serikali inaendelea na utafiti ili kuwepo na uhifadhi mzuri wa matukio ya ukatili na namna ya kukabiliana nayo ili kumaliza matukio hayo kwa siku zinazo kwa kuwa kwa sasa hakuna takwimu zilizohifadhiwa vizuri.
More Stories
Changamoto za mabadiliko ya tabianchi zinavyoweza kuathiri ustawi wa familia,watoto
Wanawake Mabogini wajizatiti kuvunja ukimya,usiri vitendo vya ukatili
Siku ya Kimataifa ya Chui wa Kiarabu