Na Waandishi Wetu, TimesMajira Online, Dar es Salaam
SERIKALI imetoa muda wa wiki mbili kwa wakazi wa eneo la Kijijini Kata ya Kawe, Mtaa wa Mbezi Beach B, Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam kuwa ufikapo muda huo wawe wameondoka eneo hilo kwa hiari yao.
Agizo hilo limetolewa mwishoni wiki iliyopita na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, alipokutana na wakazi wa eneo hilo alipokuwa akitembelea maeneo mbalimbali akiwataka wakazi wa wilaya hiyo kuchukua tahadhari ya mvua zinazoendelea kunyesha, hususani kwa wakazi wa mabondeni.
Mtambule alisema ni vyema wakazi wa eneo hilo wakahama kwa hiari yao, kwani wamekuwa wakiishi kinyume cha sheria kutokana na biashara haramu ambazo zimekuwa zikifanywa na watu hao.
Aidha, alisema eneo hilo ni hifadhi ya barabara, hivyo taratibu zingine za kimiundo mbinu zinatakiwa kufanyika.
Alisema imegundulika kuwa wapo baadhi yao wamejenga vibanda hivyo na kuvipangisha, jambo ambalo ni kinyume cha sheria na kwamba tayari ameagiza Jeshi la Polisi kuwachukulia hatua.
“Kutokana na maombi yenu ya kutaka kupewa wiki mbili za kuhama na kwa kuwa Serikali yetu ni sikivu, natoa muda wa siku 14 wakazi wote wa Kijijini muwe mmeshahama kwa hiari yenu ili taratibu nyingine za kimiundombinu ziendelee na mkikaidi maagizo basi tutawachukulia hatua kali,” alisema Mtambule.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alipoulizwa hivi karibu kuhusiana na kinachoendelea Kijijini, alisema anatambua uwepo wa eneo la Kijjini Mbezi Beach B, kata ya Kawe, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam kuwa ni eneo hatarishi kwa wakazi wa eneo hilo kutokana na baadhi ya watu wanaoishi eneo hilo kujihusisha na vitendo viovu.
Hata hivyo, alisema wanafanya utaratibu wa kujua namna gani watatatua tatizo liliopo mtaa huo, kwani kuna watu wengine ni wazuri lakini hawana makazi ya kuishi.
Alisema, tayari walishaongea na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ambao mtaa huo upo kwenye eneo la nyumba zao ili wajue jinsi ya kutatua tatizo la hao watu ikiwemo kuwahamisha na kuwatafutia makazi.
Gazeti la Majira hivi karibuni lilifika katika eneo hilo dogo la Kijijini na ukashuhudia maovu yanayoendelea ambayo yamehalalisha vitedo vya uvunjifu wa sheria kama sehemu ya maisha ya wakazi hao.
Katika eneo hilo, zinaishi kaya takribani 30 hadi 40, wakazi wa eneo hilo, wanaishi kwenye vibanda vya mabati, ambavyo ndiyo makazi yao ya kudumu na familia zao kwa takriban miaka 30.
Makazi hayo huyatumia kama sehemu zao za kufanyia biashara haramu, ambazo wao wamezihalalisha. Biashara zinazofanyika katika eneo hilo ni uuzaji wa dawa za kulevya, bangi, pombe haramu ya gongo, pombe za kienyeji na ngono ya nipe nikupe (kununua).
Kufuatia malalamiko wa wananchi kuhusiana na eneo hilo, gazeti la Majira lilipiga kambi katika eneo hilo kuchunguza yanayoendelea, ambapo wao hawaoni kama ni uvunjifu wa sheria, bali ni biashara haramu.
Biashara ya ngono ya nipe nikupe katika eneo hilo, inahusisha wanawake na wasichana wenye umri mdogo. Kinachofanyika ni maelewano na baada ya hapo, maisha yanaendelea.
Wakati wakazi wanaoishi eneo la Kijijini wakiwa wameridhika na maisha ya eneo hilo, baadhi ya wananchi waliokuwa na nyumba za kudumu jirani ya Kijijini wamezikimbia na kwenda kuishi kwingineko, kwani eneo hilo sio salama kwao na malezi ya watoto na katika suala la maadili.
Mbali na hilo, pia eneo hilo limeonekana kuwa ni hatari kwa watoto chini ya miaka 18. Mbali na lugha chafu zinazozungumzwa na wanaofika kupata huduma, lakini kibaya zaidi watu hao wamesahau kwamba kuna vyombo vya dola.
Baada ya Gazeti Huru la Majira kufika eneo hilo, lilishuhudia na kujiridhisha kufanyika kwa biashara haramu na kujionea jinsi watoto wanaoishi jirani wanavyokabiliwa na tishio kubwa la kimaadili.
Mmoja wa wauza dawa za kulevya anayejulikana kwa kwa jina la Mengi, au Baba Bodo, anakiri kufanya biashara hizo, akidai ndiyo inayomuingizia kipato cha kuendesha familia yake.
“Mimi nipo hapa na mke wangu, tunaendesha maisha kupitia biashara hii na sio mimi tu, wakazi wengi wa eneo hili hii ndio biashara yao (kuuza dawa za kulevya),” alisema Bodo.
Naye mfanyabiashara wa nguo za mitumba (jina limehifadhiwa) ni mmoja wa wavutaji bangi katika eneo hilo, ambaye alidai kuwa mara nyingi huwa anafika hapo kwa ajili ya kuvuta na baadaye anaondoka.
Anakiri kuwa eneo hilo sio salama kukaa muda mrefu, ndiyo maana anawahi kuondoka.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi