September 30, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakasuvi ataka UVCCM kujitoa zaidi kutumikia Chama

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoani hapa wametakiwa kujitoa zaidi kutumikia chama chao katika shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo kuwa tayari kukitumikia katika mataifa mbalimbali.

Hayo yamebainishwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa na Mwenyekiti wa Chama Mkoa wa Tabora, Hassan Wakasuvi alipokuwa akihutubia umati mkubwa wa wanaCCM katika kilele cha sherehe za miaka 46 ya kuzaliwa CCM iliyofanyika Kimkoa jana katika uwanja wa kata ya Bukoko Wilayani Igunga.

Alisema vijana ni nguzo kubwa ndani ya chama hivyo wanapaswa kujitoa zaidi kukitumikia ili kiweze kupiga hatua kubwa kimaendeleo kwa manufaa ya wanachama na wananchi kwa ujumla.

Alisisitiza kuwa Jumuiya hiyo ina nafasi ya kufanya mambo makubwa kinachotakiwa ni kuwa na mipango mizuri ya maendeleo na kusimamia utekelezaji wake kwa dhati.

Wakasuvi aliwataka kutokuwa chawa wa wagombea fulani tu bali waendelee kujitoa zaidi kwa chama chao ikiwemo kuwa tayari kukitumikia ndani na nje ya mipata ya nchi yao.

Aidha alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Igunga Nicholous Ngassa kwa uamuzi wake wa kujenga Ofisi za CCM katika kata zote zikiwa na Ofisi za Jumuiya za Vijana, Wanawake na Wazazi na ukumbi wa mikutano.

‘Najua kila wilaya ina mipango yake ya kujenga Ofisi za chama katika kila kata, nashauri miradi hiyo ijengwe katika kata moja moja na kumalizika kabla ya kuendelea na kata nyingine ili msikwame na kuwa na magofu tu’, alisema.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Mohamed Nassoro Hamdan (Meddy) alimpongeza Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia vizuri chama hicho.

Aliongeza kuwa tangu kuzaliwa kwake Februari 5, 1977, CCM imeendelea kusimamia dhamira yake ya kulinda amani na utulivu wa nchi kwa vitendo hadi sasa, ikiwemo kusimamia haki na usawa wa wananchi.

Alieleza dhamira nyingine ni kuwakomboa wanachama na wananchi kwa ujumla kisiasa na kiuchumi na kulinda na kutetea Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kuongeza kuwa CCM madhubuti ndiyo imepeleka kudumu Muungano.

Naye Katibu wa CCM Mkoa wa Tabora Elias Mpanda alisema katika wiki ya maadhimisho hayo jumla ya wanachama 2521 kutoka vyama vya upinzani wamerudi CCM baada ya kuridhishwa na kazi nzuri inayofanywa na Rais Samia.

Alibainisha kuwa kati ya wanachama hao 1941 wamesajiliwa katika mfumo wa kielektroniki, na wanachama 652 wamejiunga UVCCM, 342 Jumuiya ya Wazazi na 362 Jumuiya ya Wanawake.

Viongozi na Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoa maeneo mbalimbali Mkoani Tabora wakimsikiliza Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora Hassan Wakasuvi (hayuko pichani) wakati wa kilele cha Maadhimisho ya miaka 46 ya kuzaliwa kwa chama hicho yaliyofanyika jana Kimkoa katika kata ya Bukoko Wilayani Igunga Mkoani Tabora. Picha na Allan Vicent