December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakandarasi, Wazabuni wanatakiwa kujengewa uwezo katika kazi zinazotolewa na Serikali

Na Penina Malundo, Timesmajira

SERIKALI imesema kuwa wakandarasi na wazabuni wa ndani ya nchini wanapaswa kujengewa uwezo katika kazi wanazozifanya ili kuweza kupata kipato,kuongeza fursa za ajira kwa wananchi,kushiriki kwenye kuongeza ujuzi na kuongeza mitaji yao katika kazi zinazotolewa na Serikali.

Ameyasema hayo jana jijini Dar es Salaam Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha,Elijah Mwandumbya wakati wa mkutano ulioandaliwa na Benki ya Duniani kwa kushirikiana na Mamlaka za kudhibiti ununuzi wa umma Tanzania Bara (PPRA) na Visiwani uliowakutanisha Jumuiya ya Wazabuni.

Amesema kupitia mkutano huo,Serikali itaweza kuendelea kutekeleza mikakati mbalimbali kama wao ni wahusika wakuu wa ununuzi wa umma nchini ikiwemo kufanya kazi kwa ukaribu na wazabuni pamoja na wakandarasi kwa lengo la kujifunza na kuona changamoto mbalimbali zinazojitokeza na kisha kuzifanyia kazi.

Amesema katika kutimiza mikakati hiyo mwaka 2023 Serikali baada ya kupata kibali cha bunge iliweza kufanya maboresho na kuanzisha sheria mpya ya ununuzi wa umma ambayo imetoa fursa zaidi kwa watanzania.

”Pia tumekwenda mbali zaidi kutasfiri namna wanavyowekea upendeleo kwa watanzania hasa kwenye maeneo yanayotumia rasiliamari au malighafi nchini na yale yanayoajili watanzania kuna upendeleo wao,”amesisitiza.

Aidha amesema katika kutekeleza bajeti ya serikali,asilimia kadhaa inayotoka katika bajeti ya serikali inakwenda kwenye ununuzi na ugavi wa umma ambapo kiwango hiki kinapita mikono ya wazabuni na wakandarasi.

”Katika kutekeleza bajeti hiyo tunashirikiana na taasisi mbalimbali ikiwemo benki ya dunia katika kuhakikisha miradi inayofadhiliwa na benki hiyo ya dunia inahakikisha ushiriki wa watanzania inakwenda zaidi katika eneo hilo ili kuhakikisha malengo yanafikiwa ipasavyo,”amesema.

Mkutano ulioandaliwa na Benki ya Duniani kwa kushirikiana na mamlaka za udhibiti ununuzi wa umma Tanzania Bara na Visiwani lengo ni kukutana na Jumuiya ya wazabuni ambao wanahitaji kufanya kazi katika miradi inayofadhiliwa na Benki ya Dunia.

Amesema sababu imeonekana kwa kiasi kikubwa wadhabuni wa ndani watanzania wamekuwa hawapati zabuni za kutosha katika miradi inayofadhiliwa na benki kuu.

Kwa Upande wake Kamishna anayesimamia Maendeleo ya Sera za Ununuzi wa Umma na Ugavi kutoka Wizara ya Fedha,Fredrick Mwakibinga amesema mkutano huo ni wa kuwakutanisha wakandarasi na wazabuni kutoka kampuni mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha kampuni za kitanzania zinapata tenda katika miradi inayofadhiliwa na Benki ya dunia pamoja na washirika wengine wa kimaendeleo.

Amesema mkutano huo umegusa maeneo mbalimbali ya majadiliano ikiwemo namna ya kupata fursa ya kupata miradi hiyo,Changamoto wanazokabiliana nazo wakandarasi pamoja na kuona namna ya zabuni zinavyogawanyishwa kwa wakandarasi wazawa na wa nje.

Amesema bado kuna changamoto mbalimbali zinawakabili wazabuni wa ndani ikiwemo suala la elewa kila upande wa Wazabuni,kujenga uwezo wa wazabuni wa ndani,pamoja na masuala ya uwezeshwaji kimitaji kupata mikopo katika mabenki.

Naye Meneja Uendeshaji, wa Benki ya duniani nchini, Milena Stefanova amesema miradi yao inakuwa na masharti kwa sababu wanataka ijengwe kwa kuzingatia sifa na vigezo.”Lengo ni kukutana na wazabuni ambao wana interest ya kufanya kazi katika miradi ambayo inakadiriwa na Benki ya Dunia hivyo tumekutana leo ili kujua changamoto ni nini na wazabuni wa ndani pia waweze kushiriki,” amesema.