May 30, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakandarasi wa umeme wasio na leseni waonywa

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online – Mwanza

Wakandarasi wa kufunga mfumo wa umeme kwenye majengo wametakiwa kuacha kufanya kazi bila kuwa na leseni kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), huku wakihimizwa kuzingatia sheria na kuacha kutumia leseni za wenzao.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Magu, Joshua Nassari, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, wakati wa semina ya kuwajengea uwezo wakandarasi wa umeme na wadau wa sekta hiyo kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mwanza. Semina hiyo iliandaliwa na EWURA Kanda ya Ziwa na kuwahusisha zaidi ya wakandarasi 100.

“Kazi ya ufungaji wa mfumo wa umeme ni muhimu,inagusa maisha ya watu. Ni kosa kutumia leseni ya mtu mwingine au kufanya kazi bila leseni kutoka EWURA,” amesisitiza  Nassari.

Meneja wa EWURA Kanda ya Ziwa, George Mhina,amesema baadhi ya majanga ya moto yaliyowahi kutokea katika maeneo mbalimbali kama shule, masoko na nyumbani, yamesababishwa na ufungaji duni wa mifumo ya umeme unaofanywa na watu wasio na sifa wala leseni.

“Kuna wakati watu wanatumia vifaa duni kwa lengo la kujinufaisha, lakini madhara yake ni makubwa. Tunawakumbusha mafundi kuwa kazi yao ni taaluma inayohitaji kufanywa kwa weledi na kwa kufuata sheria.EWURA inatoa elimu kwa vyuo vya ufundi ili kuandaa mafundi bora na wenye weledi,”amesema Mhina.

Mhina amesema hadi sasa EWURA imesajili wakandarasi 972 kwa Kanda ya Ziwa, ambapo zaidi ya 400 wapo Mwanza, 140 Kagera, na 99 Simiyu. 

Mhandisi Mwandamizi  wa umeme kutoka EWURA Kanda ya Ziwa, Jonathan Elizeus, amesema wapo mafundi wasiosajiliwa wanaotumia majina ya mafundi wenye leseni kuwasilisha maombi TANESCO, hali inayohatarisha usalama wa wananchi. Alisisitiza kuwa mtu anayefanya kazi bila leseni akibainika atachukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo faini au kifungo.

Hata hivyo amesema, utafiti wa EWURA unaonyesha kuwa kati ya kazi 10 za ufungaji wa mifumo ya umeme, ni tatu au nne pekee ndizo zinafanywa na mafundi wenye leseni huku asilimia 60 zinafanywa na mafundi wasio na leseni.

 Kaimu Ofisa Uhusiano Huduma kwa Wateja wa TANESCO Mkoa wa Mwanza, Nyanso Choholo, amesema shirika hilo limeanzisha mfumo wa neConnect ambao unawaorodhesha wakandarasi wote wa umeme ili kusaidia wateja kuchagua mafundi waliothibitishwa.

Grace Mang’ombe, mwanafunzi wa VETA Mwanza anayesomea fani ya umeme,amedema semina hiyo imemfungua macho kuhusu umuhimu wa leseni na nafasi ya wanawake katika tasnia hiyo,ambayo inafursa nyingi ikiwemo kujiajiri mwenyewe.

Naye Stephen Hosea kutoka KANSH Ltd, ameeleza kuwa mafunzo yamewasaidia kuelewa vipimo vinavyopaswa kuzingatiwa katika ufungaji wa mifumo ya umeme kwani mafundi wengi wananchangamoto ya vipimo.