April 2, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wajumbe wa ALAT Tanga wampongeza Dkt.Samia kwa mradi wa maji Miji 28

Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Korogwe

WAJUMBE wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) Mkoa wa Tanga wamempongeza Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi mkubwa wa Mradi wa Maji Miji 28 unaotekelezwa kwenye miji minne ya Handeni, Korogwe, Muheza na Pangani.

Wakizungumza kwenye majumuisho Ukumbi wa Halmashauri ya Mji Korogwe mara baada ya kutembelea mradi huo eneo la chujio Machi 28,2025 lililopo eneo la Kata ya Mswaha wilayani Korogwe, walikubaliana kwa kauli moja kuwa Rais Dkt. Samia anafanya kazi kubwa na nzuri ya kujenga miradi ambayo ina tija kubwa kwa wananchi.

Mjumbe kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kwemshasha,Anuary Abdassi alisema mradi huo wa miji 28,ambapo kwa Mkoa wa Tanga wamepata miji minne, utakuwa mkombozi kwa wananchi wengi watakaofaidika na mradi huo, na kutaka ALAT iweze kutoa pongezi kwa Rais Dkt. Samia kwa kazi nzuri anayofanya.

Mjumbe mwingine ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto na Diwani wa Kata ya Magamba Mathew Mbaruku, alisema mradi huo unahitaji kupata maji kwa siku lita milioni 52, na kwa kipindi cha miaka 20. Lakini hofu yake ni uharibifu wa mazingira unaofanywa na binadamu, hivyo labda malengo hayo yasiweze kutimia.

“Mradi huu unatakiwa kutoa maji lita milioni 52 kwa siku. Na kati ya lita hizo, lita milioni 51 zitawafikia wananchi, na lita milioni moja itapotelea kwenye chujio. Hoja yangu, kuwe na mikakati ya kulinda mazingira Mto Pangani kwa kuhakikisha mto huo unadumu na kuwa endelevu. Lakini nataka kujua, ni kweli lita milioni 52 za maji zitapatikana kila siku kwa kipindi chote kwa mwaka mzima!” alihoji Mbaruku.

Mwenyekiti wa ALAT Mkoa wa Tanga, na Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga Abdulrahman Shiloow alimtoa wasiwasi Mbaruku na wajumbe wengine wa ALAT kuwa mradi huo ulipofanyiwa Upembezi Yakinifu na Usanifu, ulifanyika kwa kuangalia majira ya mwaka mzima, iwe kiangazi ama masika, dakio la mradi huo litaendelea kupata maji lita milioni 52 kwa siku.

Akitoa taarifa kwa Wajumbe wa ALAT kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Handeni Trunk Main (HTM), Mhandisi Yohana Mgaza, Msimamizi wa Mradi Michael Victorian alisema, Mradi wa Maji wa Miji 28 unahusisha kutoa maji Mto Pangani katika eneo la Kata ya Mswaha kwenda katika miji ya Handeni, Korogwe, Muheza na Pangani, ambapo
unatekelezwa na Mkandarasi M/s JWIL INFRA Ltd kwa gharama ya dola za
Marekani 81,142,931 na unatekelezwa kwa kipindi cha miezi 32, ambapo
unatarajiwa kukamilika Desemba 10, 2025.

“Mradi huu unasanifiwa na
kujengwa (Design and Build).
Mradi huu umelenga kuongeza uwezo wa kuzalisha maji kutoka mita za ujazo 5,500 (lita milioni 5,500) kwa siku hadi mita za ujazo 52,000 (lita milioni 52) kwa siku. Lengo ni kutimiza mahitaji ya maji kwa miaka 20 ijayo kwa watu watakaoweza kufikiwa na huduma hiyo ya maji katika miji ya Korogwe, Handeni, Muheza na Pangani. Kazi zilizopangwa kufanyika (Scope of Works). Ujenzi wa dakio (water intake) lenye ukubwa wa lita milioni 52 kwa siku kutoka
katika chanzo cha Mto Pangani katika kijiji cha Mswaha darajani.

“Ujenzi wa chujio (Water Treatment Plant) lenye ukubwa wa lita milioni 51 kwa siku, ujenzi wa vituo viwili vya kusukuma maji katika maeneo ya Kwamatuku na Sindeni (Booster pumping station at Kwamatuku & Sindeni), ulazaji wa bomba kuu la maji lenye kipenyo kati ya milimita 150 hadi 800 lenye urefu wa kilomita 188, ujenzi wa matenki manane (8) ya kuhyifadhia maji yenye ukubwa tofauti (6 GSR & 2 ESR) kuanzia lita 200,000 hadi 2,000,000 katika maeneo tofauti” alisema Victorian.

Victorian alisema tenki la Vibaoni lililopo Handeni mjini lina ujazo wa lita milioni mbili, Bongi (Handeni) lita milioni moja, Segera (Handeni) lita 500,000, Kwafungo wilayani Muheza, lita 500,000, Kilulu (Muheza) lita milioni mbili, Ubangaa wilayani Pangani lita 200,000, Madanga (Pangani) lita 200,000 na Boza (Pangani) lita 500,000

“Ulazaji wa mabomba ya usambazaji maji yenye urefu wa kilomita 100, yenye
vipenyo tofauti kuanzia mlimita 75 hadi milimita 500. Kazi ambazo zimefanyika, ujenzi wa dakio (water Intake 52MLD) unaendelea. Hata hivyo, changamoto iliyotokana na mtiririko mkubwa wa maji, na maji kujaa sehemu ya ujenzi wa dakio la maji, imesababisha kupunguza kasi ya ujenzi.Ujenzi wa chujio (WTP 51MLD) kazi inaendelea na upo katika hatua tofauti za ujenzi” alisema Victorian, ambapo mradi wote umefikia asilimia 64.

Wajumbe wa ALAT walitembelea miradi mingine mitano kwenye Halmashauri ya Mji Korogwe ikiwemo vyumba vipya vya madarasa matatu na choo Shule ya Msingi Kwakombo, Zahanati ya Lwengera- Darajani na vijana wajasiriamali wa bajaj waliokopeshwa na halmashauri hiyo sh. milioni 40.