January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ramani ya Mkoa wa Shinyanga

Wajumbe kiboko, wawashugulikia Madiwani 7 katika majimbo mawili

Na Sulleiman Abeid, TimesMajira Online, Shinyanga

MADIWANI saba katika majimbo ya Shinyanga Mjini na Solwa mkoani Shinyanga wameangushwa katika uchaguzi wa kura za maoni.

Kwa upande wa Jimbo la Shinyanga Mjini madiwani watatu ambao ni Lucas Magige kata ya Old Shinyanga, Agnes Machiya, Kata ya Kolandoto na Daniel Mathemu kata ya Ibinzamata wameangushwa kwenye uchaguzi huo wa kura za maoni.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Agnes Bashemu katika Kata ya Ibinzamata mgombea aliyeongoza ni Ezekiel Sabo aliyepata kura 22 ambapo diwani anayemaliza muda wake, Daniel Mathemu alipata kura 12 na Mohamed Mgendi kura 04.

Pia katika Kata ya Kolandoto, diwani anayemaliza muda wake, Anges Machiya alishindwa kupata ushindi baada ya kupata kura 27, huku mpinzani wake aliyeongoza, Mussa Elias akipata kura 41 na Sheka Ngusa akipata kura 12.

Diwani mwingine anayemaliza muda wake aliyeangushwa kwenye kinyang’anyiro cha kura za maoni ni wa kata ya Old Shinyanga Lucas Magige aliyepata kura 29 ambapo alishinda ni Charles Lyota aliyepata kura 32 na Silas Machela akiambulia sifuri.

Katibu Bashemi amesema madiwani wengine 13 katika Jimbo la Shinyanga mjini lenye kata 17 wamefanikiwa kuongoza katika kura hizo za maoni akiwemo Gulamu Mukadamu, Mstahiki Meya aliyemaliza muda wake ambaye aliongoza katika kata yake ya Mjini Shinyanga kwa kupata kura 25 huku mpinzani wake wa karibu Salumu Kitumbo akipata kura 10 na Nassor Warioba kura nne.

Kwa upande wa Jimbo la Solwa lenye kata 26, Katibu wa CCM wa wilaya ya Shinyanga vijijini, Erenestina Richard amesema madiwani wane wameshindwa katika kura za maoni akiwemo diwani wa kata ya Usule, Amina Kulindwa aliyepata kura 31 huku mshindi katika kata hiyo, Ezekiel Seleli akipata kura 40 na Amos Lugobi kura 13.

Erenestina amesema katika kata ya Lyabukande diwani wa zamani, Joseph Misiri aliangushwa baada ya kupata kura 34 na mshindi katika kata hiyo, Luhende William akipata kura 110 na katika kata ya Mwakitolyo, Masalu Nyese aliongoza kwa kura 91, diwani wa zamani, Limbe Limbe alipata kura 39 na Zephania Mlyashi akipata kura 19.

Diwani mwingine aliyeangushwa kwenye kura za maoni ni wa kata ya Imesela James Mlekwa aliyepata kura nne huku mshindi katika kata hiyo Sethi Msangwa akipata kura 41 na Juma Kayungo aliyepata kura 16 ambapo madiwani wengine wa zamani katika kata 22 waliweza kuongoza kwenye kura hizo za maoni.