Na Allan Vicent, Kasulu,timesmajira,online
VIKUNDI vya wajasiriamali zaidi ya 700 kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini vimejitokeza kushiriki maonesho ya uzalishaji bidhaa ambayo mwaka huu yamefanyika Kitaifa wilayani Kasulu Mkoani Kigoma.
Wakizungumza na timesmajira kwa nyakati tofauti kutoka katika uwanja wa Umoja wilayani Kasulu ambako ndiko maonesho hayo yamefanyika baadhi ya akinamama wajasiriamali walisema kuwa maonesho hayo yamewapa manufaa makubwa.
Mjasiriamali kutoka Mkoani Tabora Ashura Mwazembe ambaye pia ni Mratibu wa Wajasiriamali wa Mkoa huo amesema kuwa wameshuhudia ubunifu mkubwa wa bidhaa zinazozalishwa na vikundi mbalimbali hivyo kujifunza mambo mengi.
Amebainisha kuwa elimu, ubunifu na matumizi ya teknolojia ambayo imekuwa ikitolewa imeongeza chachu kubwa ya kuboreshwa kwa bidhaa zinazolishwa nchini hivyo kufanya maonesho hayo kuwa kivutio kikubwa kwa watazamaji.
‘Tunaipongeza serikali kupitia Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo nchini (SIDO) kwa kutoa elimu na mafunzo ya teknolojia bora ya uzalishaji bidhaa na mikopo nafuu kwa vikundi vya wajasirimali, wametuinua zaidi’, amesema.
Wazalishaji wa bidhaa za vyakula Mwamvua Issa na Elizabeth Kayanda kutoka Tabora wamesema kuwa licha ya kujipatia fedha kwa kuuza bidhaa zao, maonesho hayo yamewafungulia mlango wa masoko.
Mjasiriamali Saidat Suleiman kutoka Unguja, Zanzibar amesema licha ya bidhaa zake kupata wateja wengi kutoka mikoa mbalimbali pia amepata marafiki wengi wa kibiashara na kuahidi kuwa ataendelea kushiriki katika maonesho mengine.
Mwenyekiti wa Chama Cha Wafanyabiashara Wanawake (TWCC) Mkoani Tabora Amina Madereka amesema kuwa maonesho hayo ni fursa muhimu sana ya kutangaza bidhaa na kujifunza teknolojia inayotumiwa na wengine.
Amepongeza waandaaji (SIDO) kwa kualika wadau kutoka ndani na nje ya nchi kuja kushuhudia bidhaa zinazolishwa hapa nchini, hili litasaidia kupanua wigo wa masoko kwa bidhaa zote.
Meneja wa SIDO Mkoani Tabora Samweli Neligwa amesema hamasa na maandalizi mazuri ya maonesho hayo imekuwa chachu kwa watu wengi kushiriki, zaidi ya wajasiriamali 700 wameleta bidhaa zao mwaka huu tofauti na miaka ya nyuma.
Amesema mwaka huu Mkoa wa Tabora umeongoza kwa kuleta washiriki wengi zaidi (107) kuliko mikoa mingine yote, mwaka juzi Mkoa huo ulileta washiriki 52 na kwa nchi nzima washiriki walikuwa 500.
Ameahidi kuwa wataendelea kutoa elimu na mafunzo kwa vikundi vyote vya wazalishaji ili kuhakikisha bidhaa wanazozalisha zinakuwa na ubora unaotakiwa katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
More Stories
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari
Gridi za Tanzania, Kenya kuimarisha upatikanaji wa umeme