December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wajasiriamali washauriwa kuanzisha viwanda vidogo

Na Magesa Magesa,Arusha

WAJASIRIAMALI nchini wametakiwa kujikita kuanzisha
viwanda vidogo ili kuuunga mkono juhudi za Serikali za ujenzi wa
Tanzania ya viwanda.

Pia wameshauriwa kuzalisha bidhaa zenye ubora na zenye
viwango ambazo zitauzwa kwa gharama nafuu ndani na nje ya nchi.

Ushauri huo umetolewa na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo Vidogo nchini (SIDO), mkoani hapa, Nina Nchimbi alipokuwa akifunga
mafunzo ya wiki moja ya usindikaji wa bidhaa za chakula kwa
wajasiriamali wadogo 32 yaliyofanyika katika ofisi za shirika hilo juzi.

Amesema endapo watajikita katika kuanzisha viwanda vidogo licha
ya wao wenyewe kujikwamua kiuchumi pia itasaidia kuongeza ajira kwa
jamii, kwani ukosefu wa ajira imekuwa ni changamoto kubwa hususani kwa
vijana hapa nchini

“Sisi SIDO tupo kwa ajili ya kuwasaidia wajasiriamali mbalimbali
kutatua changamoto zinazowakabili ili mfikie
malengo mliyojiwekea,tunatoa wito kwenu hakikisheni kuwa mnatumia
kikamilifu mafunzo tuliyowapatia kwa vitendo kuanzisha
viwanda,” amesema Nina

Amewataka wajasiriamali wawe wamiliki wabunifu ikiwa ni pamoja
na kuchangamkia fursa zilizopo hapa nchini hususani kipindi hiki
ambacho Tanzania imekuwa nchi ya uchumi wa kati,ikiwa ni pamoja na
kuhakikisha kuwa wanasajili bidhaa wanazozalisha

Awali akimkaribisha Meneja huyo wa SIDO,Mratibu wa mafunzo hayo,Bahati
Mkopi amewataka wahitibu hao kuhakikisha wanazingatia mafunzo
waliyopatiwa na kwamba SIDO itaendelea kuwaunganisha na taasisi
mbalimbali za kifedha kwa ajili ya kupata mikopo ya kukuza mitaji yao
pamoja na kuwapatia mashine mbalimbali.

Mmoja wa wahitimu wa mafunzo hayo, Doris Mmari aliwapongeza SIDO
kwa mafunzo hayo ambapo aliiomba iongezew muda wa mafunzo.

aLITAJA changamoto kubwa wanayokabiliana nayo katika kuanzisha viwanda
kuwa ukiritimba pindi wanapotafuta vibali katika mamlaka husika.

Aliongeza kuwa uhaba wa mitaji,bei kubwa za malighafi ambazo nyingine
hupatikana nje ya nchi imekuwa ni changamoto kubwa kwao ikiwa ni
pamoja riba kubwa wanazotozwa na taasisi za kifedha.