Mwandishi wetu, Timesmajira Online
BAADHI ya wajasiriamali wa kada mbalimbali kutoka wilaya tano za Mkoa wa Dar-es-Salaam wametoa tamko lenye maazimio sita, ikiwemo kuwataka Watanzania kujiepusha na vitendo vya vurugu vinavyoweza kuliingiza taifa katika uvunjifu wa amani.
Tamko hilo limetolewa jijini Dar-es-Salaam wakati wajasiriamali hao wakizungumza na waandishi wa habari kufuatia ushirikiano wao na taasisi ya MECIRA ambayo imekuwa ikifanya kazi ya kutoa elimu ya uraia kwa wafanyabiashara wadogo wadogo.
Wamesema kuwa machafuko hayaleti tija wala suluhu ya kudumu kwa changamoto za kijamii na kiuchumi, bali husababisha hofu, hasara,kudorora kwa shughuli za uzalishaji mali na biashara.
Akisoma tamko hilo kwa niaba ya wajasiriamali hao Suleiman Said mfanyabishara ndogo ndogo kutoka Ilala, amesema wanapinga wito wowote unaotolewa na wanaharakati wa ndani na nje ya nchi wanaohamasisha vurugu kwa maslahi binafsi, hali ambayo husababisha taifa kuingia katika machafuko na hofu miongoni mwa wananchi.
“Tupo tayari kupaza sauti kupigania ustawi wa taifa kwani bila amani hakuna biashara, ajira wala maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa watanzania,”amesema Said.
Amesema kuwa watawapinga wanasiasa wote wanaotumia vurugu, matusi na uchochezi kama njia ya kutimiza malengo yao ya kisiasa kinyume na misingi ya demokrasia na maadili ya taifa.
Pia amesema dhamira yao ni kupinga propaganda zinazotumia kizazi cha Gen-Z kuhalalisha vurugu, fujo na ukosefu wa maadili, huku wakisisitiza kuwa kizazi hicho ni nguvu kazi muhimu na mustakabali wa taifa.
Lucy Piter,mjasiriamali kutoka Tandika amesema matukio ya vurugu yaliyotokea Oktoba 29, 2025, yamekuwa somo kwa Watanzania, akisisitiza kuwa uvunjifu wa amani hauwezi kuleta maendeleo wala kutoa suluhu ya kudumu kwa changamoto zilizopo.
Kwa upande wake Hussein Bambe mfanyabishara kutoka Ubungo,amelaani vitendo vya uchochezi na kuwataka vijana wa Kitanzania kutowasikiliza watu wanaohamasisha vurugu kwa maslahi ya kisiasa au binafsi.
Amesema wataendelea kupaza sauti kupinga wanaharakati wanaojificha nje ya nchi, wanamitandao wanaoeneza chuki, wanasiasa wanaohamasisha vurugu pamoja na viongozi wa dini wanaoingiza siasa katika majukwaa ya kiimani.
Mzee Omary Suleiman, mfanyabiashara wa soko la Kinondoni, amesema ni wajibu wa kila Mtanzania kuhakikisha matukio kama hayo hayajirudii tena ili Tanzania iendelee kubaki salama yenye amani na utulivu.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi