February 2, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waislamu wamuombea dua Rais Samia,wasisitiza umoja

Na Daud Magesa, Timesmajira Online,Mwanza

WAISLAMU mkoani Mwanza, kwa kushirikiana na viongozi wa dini na siasa,wamemuombea dua Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,huku wakihimiza umoja na maendeleo.

Dua hiyo imefanyika nje ya Msikiti wa Sheikh Abubakar Zubeir Bin Ally, na kuhusisha viongozi wa dini,waumini wa dini ya Kiislamu, wananchi wakiwemo viongozi na wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu Tanzania (JUWAKITA), Amina Masenza,ameeleza kuwa Rais Samia amekuwa mkombozi kwa Watanzania, hasa wanawake, kutokana na miradi ya maendeleo aliyotekeleza ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya maji, umeme na huduma bora za afya.

“Wanawake wamepata unafuu kutokana na miradi ya maji,ametutua ndoo kichwani,ameboresha huduma za afya na sasa tunapata huduma kwa urahisi, pia ameteua wanawake katika nafasi mbalimbali za uongozi,”.

Masenza ameongeza kuwa, ni muhimu kwa Watanzania kuendelea kumuombea dua ili aendelee kufanya kazi nzuri kwa ajili ya taifa.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Nyamagana,Peter Begga,amesema,miradi ya kimkakati kama daraja la Kigongo-Busisi limekamilika na SGR inakwenda kwa kasi,jambo ambalo lilinaonekana kama ndoto.

Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Hassan Kabeke,amesisitiza kuwa kumuombea Rais Samia ni wajibu wa kila Mtanzania, na kwamba dua ni nguvu kubwa inayoweza kuimarisha amani na umoja wa taifa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, amewapongeza Waislamu mkoani humu kwa kuonesha mshikamano na upendo kwa Rais Samia.

Amesisitiza kuwa dua ni chakula cha nafsi na roho,inasaidia viongozi kuwa na nguvu ya kupambana na changamoto mbalimbali wakiwemo maadui wasiowafahamu .

Dua hiyo imeonesha mshikamano wa kitaifa, na imesisitiza kuwa maendeleo ya kijamii yanaweza kupatikana tu kupitia ushirikiano wa wananchi,viongozi wa dini na siasa.