Na Hadija Bagasha,TimesMajira Online, Tanga
Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Tanga Juma Luwuchu amewataka waislamu kutumia mwezi mtukufu wa ramadhani kuliombea Taifa ili amani iliyopo iendelee kudumu wakati wote.
Sheikh Luwuchu ametoa kauli hiyo wakati wa hafla ya futari iliyoandaliwa na benki hiyo na kuwashirikisha watu wenye mahitaji maalumu, viongozi wa dini na viongozi wa kiserikali.
Sheikh Mkuu Luwuchu amesema kuwa ni wakati wa kuendelea kufanya ibada ya kuendelea kuiombea nchi yetu ili iendelee kubaki na hali ya amani iliyopo hivi sasa.
Aidha Sheikh Luwuchu alitumia nafasi hiyi kumuombea Rais wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuendelea kuwa na afya njema ili taifa lizidi kuendelea kuwa hali ya utulivu na amani ikiwa ni pamoja na kuwatumikia watanzania ipasavyo.
Alisema wataendelea kuitambua heshima waliyopewa na benki hiyo ya kuwa Mkoa wa kwanza kufuturishwa na taasisi za kibenki.
Mkuu wa wilaya ya Tanga Hashimu Mgandilwa amewataka waislamu kuendelea na utamaduni wa mavazi wanayoyavaa katika kipindi cha mwezi mtukufu wa ramadhani huku wakiendelea kutenda mambo mema yanayompendeza Mungu
Mgandilwa ameipongeza benki hiyo kwa kuendelea kujenga mahusiano mazuri kati yao na wadau wao kwani ni miongoni mwa benki ambayo imekuwa ikijali wateja wao.
“Wengi aina ya mavazi ambayo tumeyavaa katika kipindi hiki yamekuwa ya kupendeza unaweza ukatazama watu hata mara mbili na usijue ni nani kwahio hiyo tafsiri tu ya aina ya mavazi ni tafsiri tosha ya kwamba tuendelee kudumisha niwaombe hakuna shida wafanyakazi wa crdb kila siku ya ijumaa muendelee kuvaa mavazi haya kwani ukanda mliopo unasadifu aina ya mavazi haya mliyovaa leo , “alisisitiza DC Mgandilwa.
Aliipongeza benki hiyo kwa aina ya ubunifu walioufanya ya uanzishwaji wa huduma ya Al barakah banking kwani kwenye sheria za dini ya kiislamu riba haiswii hivyo kuanzishwa akaunti inayoendana na mifumo na taratibu za kiislamu itasaidia kundi lililokuwa likiachwa nyuma kuungana pamoja nao.
Kwa upande wa benki ya CRDB Alex Ngusaru ambaye ni Mkurugenzi wa idara ya hazina kutoka benki ya CRDB amesema kuwa imekuwa ni utamaduni wa benki hiyo kushirikiana na jamii ikiwa ni mpango wa kurudisha sehemu ya faida wanayoipata kutoka kwa jamii wanayoihudumia.
Amesema kuwa futari waliyoitoa ni kwanza katika kipindi hiki cha mwezi huu wa ramadhani ambapo ni ishara tosha kuwa benki hiyo inathamini na kuupa heshma Mkoa wa Tanga.
“Ndio futari yetu ya kwanza katika kipindi hiki tumefanya niwashukuru wote kwa kuweza kujumuika nasi na ninawaahidi kuwa benki yetu ya CRDB daima itaendele kuwa tayari kushirikiana na wadau mbalimbali wa jamii nzima ya watanzania na sio katika kipindi hiki tuu bali katika nyakati zote ambazo tumekuwa tukijinasibu katika kauli mbiu inayofahamika ya kwamba ULIPO TUPO, “Amesisitiza Mkurugenzi huyo wa Hazina.
Naye meneja biashara kitengo cha Al Barakah Banking Thabit Galia aliutambulisha mfumo mbadala wa kubenki unaofuata misingi na taratibu za sheria za kiislamu kwa kufuata maadili pamoja na imani ya kiislamu na namna sahihi za kibenki.
Alisema huduma hiyo ya Al Barakah Banking ni huduma ya kwanza kupatikana nchini Tanzania katika Mikoa yote kwa benki hiyo ya Crdb inayowawezesha wateja wao kupata huduma za kiislamu za kibenki.
Alisema huduma zinazopatikana ni pamoja na kufungua akaunti, kupata mikopo iliyo ya halali na wameanza kuoa huduma hizo toka mwaka jana mwezi novemba walipozindua huduma hiyo visiwani Zanzibar hivyo alitumia nafasi hiyo kuwakaribisha wateja wao kutumia nafasi hiyo ya kuwa benki inayofuata misingi na taratibu za kiislamu.
Kwa upande wake Meneja wa kanda ya kaskazini Bi. Chiku Issa amewaomba viongozi wa dini ya kiislamu kuwafungulia milango misikitini ili waweze kuwafungulia akaunti ya kiislamu inayoendana nao.
“Tumeanzisha mfumo huu wa Al barakah banking kwa makusudi ili tuweze kuwafikia waislamu ambao walikuwa hawapati fursa za kibenki kwa kuhofia mambo mbalimbali kubwa unaomba mutuunge mkono lakini pia katika hafla hii ya futari tumejumuika na watoto wenye mahitaji maalumu 25 kati ya 50 huku wengine tukiwaandalia sadaka ya futari ambayo itakwenda kuwasaidia katika kipindi chote cha mwezi mtukufu wa ramadhani, “alisema.
Ni utamaduni wa benki hiyo kujumuika na jamii inayowahudumia wakati wa mwezi mtukufu wa ramadhani ambapo hatua hiyo inafanywa na benk ya CRDB ikiwa ni sehemu ya kurejesha sehemu ya faida waliyoipata kwa jamii wanayoihudumia.
More Stories
Bei za mafuta Novemba 2024,zaendelea Kushuka
TARURA yaomba Mkandarasi aitwe
Ilemela yakusanya bilioni 3.7.robo ya kwanza