November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Dkt.Phillis Nyimbi (katikati) akiongozana na Kamati ya Ulinzi na Usalama pamoja na Meneja wa TARURA Jiji la Mwanza, Mhandisi Mohamed Muanda ( kushoto kwake) wakati wakikagua barabara ya Nyamazobe-Kasese-Nyahingi yenye urefu wa kilomita 2.38, ambayo imetatua kero ya muda mrefu ya wakazi wa Mtaa wa Nyamazobe, Kata ya Mkolani, wilayani Nyamagana, Mwanza. Picha na Judith Ferdinand

Waishukuru Serikali kwa kuwajengea barabara

Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

Wananchi wa Mtaa wa Nyamazobe Kata ya Mkolani Wilayani Nyamagana Mkoani Mwanza wameishukuru Serikali baada ya kuwajengea barabara ya Nyamazobe-Kasese-Nyahingi yenye urefu wa kilomita 2.38, ambayo ilikuwa changamoto ya muda mrefu kwa wakazi wa maeneo hayo.

Hayo yalisemwa jana wakati wa ziara ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Nyamagana, kuhusu utekelezaji wa miradi ya barabara inayosimamiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA) Jiji la Mwanza, ambapo ziara hiyo  ilitembelewa miradi mbalimbali ikiwemo barabara katika eneo hilo, ujenzi wa daraja la Fumagila iliongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Dkt.Phillis Nyimbi.

Mmoja wa wananchi wa Mtaa wa Nyamazobe ambaye ni mtoto wa darasa la nne Junior Laurent, ameishukuru serikali ya Rais Magufuli kwa barabara hiyo kwani awali ilikuwa ni changamoto wakati wa kwenda shule na kulazimika kupanda juu ya miamba na wakati mwingine kuanguka.

Laurent anasema, usafiri ulikuwa wa shida ambao iliwalazimu kushuka chini ya mlima kwa ajili ya kufuata huduma hiyo pale wanapotaka kwenda sehemu mbalimbali, hivyo aliomba daladala zianze kupita katika maeneo hayo kwa kutumia barabara hiyo 

Faustina Selestine Mkazi wa Nyamazobe amesema, awali hapakuwa na njia wala barabara inayopitika kwa urahisi hali iliyowapa wakati mgumu hata wakati wa kutaka kusafirisha maiti iliwalazimu kubeba mpaka chini tena kwa kupita juu ya mawe na wakitaka kuleta vifaa vya ujenzi ili kuwa shida maana walilazimika kutumia watu kubeba na kuwafikishia eneo husika hali iliyosababisha gharama kuwa kubwa.

Naye Meneja TARURA Jiji la Mwanza Mhandisi Mohamed Muanda, amesema sehemu kubwa ya uanzishwaji wa mradi huo wa ujenzi imetomana na juhudi za wananchi wa mtaa huo wa kuungana na kuchangia fedha kwa ajili ya kupasua mawe ili kujenga barabara hiyo kwa ajili ya kuunga mkono jitihada za Rais katika kuleta maendeleo nchini.

Mhandisi Muanda, amesema Rais aliunga mkono jitihada za wananchi wa mtaa huo kwa kuchangia milioni 20, ambapo TARURA Jiji iliamua kuingiza barabara hiyo katika mpango kazi wake wa mwaka wa fedha wa 2018/19.