November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waipa kisogo Corona, wajimilikisha silaha

STOCKHOLM,Ripoti iliyochapishwa na Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti Kuhusu Amani (SIPRI) yenye makao yake makuu mjini Stockholm, Sweden imeonyesha matumizi jumla ya shughuli za kijeshi kwa mwaka uliopita yaliongezeka kwa karibu dola trilioni mbili licha ya janga la virusi vya corona na kudorora kwa uchumi duniani.

Kwa mujibu wa SIPRI kutokana na kuanguka kwa mapato ya ndani kile kinachoitwa mzigo wa matumizi ya kijeshi kiliongezeka kwa asilimia 2.4 kutoka asilimia 2.2 mwaka 2019.

Mtafiti wa Programu ya Matumizi ya Kijeshi kwenye taasisi hiyo, Diego Lopes da Silva amesema takwimu hizo zinaashiria kwamba janga la corona halikuathiri vyovyote matumizi ya kijeshi kwa mwaka 2020.

Serikali ya China, Marekani, India, Urusi na Uingereza zinafanya jumla ya asilimia 62 ya matumizi ya kijeshi Duniani huku kiwango cha China kikipanda kwa mwaka wa 26 mfululizo.

Wakati India ikitajwa kuwa na matumizi makubwa ya silaha, kwa sasa inaendelea kushuhudia rekodi mpya ya duniani kufuatia maambukizi mapya 352,000 ya Covid-19, wakati wimbi la pili la virusi vya corona likizidi kuudhofisha mfumo wa afya nchini humo.

Serikali za Marekani, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani tayari zimeonyesha nia ya kuisaidia India. Taifa hilo la kusini mwa Asia limeorodhesha vifo 2,812 vya Covid-19 ndani ya siku moja ikiwa ni idadi ya juu tangu kuanza kwa janga hilo.

Kwa siku tano zilizopita, India imerekodi maambukizi mapya ya kila siku ya zaidi ya 300,000. Waziri Mkuu Narendra Modi juzi alisema, janga la Covid-19 limeweza kuitikisa nchi.

India ambayo ni ya pili sasa kuathiriwa zaidi na Covid-19 baada ya Marekani, inakabiliana na wimbi la pili ambalo lilianza katikati ya mwezi wa pili.