April 19, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wahitimu wa Mafunzo ya Scout Nkasi watakiwa kuwa mwangaza kwa vijana

Na Israel Mwaisaka, Timesmajira Online,Rukwa

Katika kipindi ambacho elimu ya Tanzania inapitia mageuzi makubwa kupitia mtaala mpya wa amali, kundi la wahitimu wa mafunzo ya wakufunzi wa Scout kutoka wilaya ya Nkasi wamepewa wito kuwa mstari wa mbele katika kuwajenga vijana shuleni.

Akifunga kambi ya siku nne ya mafunzo hayo, iliyofanyika katika shule ya sekondari Nkasi, Kaimu Ofisa Elimu Sekondari wa wilaya hiyo, Fortunatus Kaguo, aliwahimiza wakufunzi hao kutumia ujuzi walioupata kuibua vipaji, kuhamasisha ubunifu, na kujenga nidhamu kwa vijana wa Scout.

“Katika zama hizi ambapo mtaala mpya wa elimu unaweka mkazo kwenye maarifa ya vitendo, mafunzo ya Scout yanapaswa kuwa sehemu ya msingi ya kulea vijana wanaoweza kusimama wenyewe katika maisha,”amesema Kaguo.

Mbali na kujifunza mbinu za kufundisha vijana, wahitimu hao walipata mafunzo ya kina kutoka kwa Mkufunzi wa Kitaifa, ALT. Edmak Mwamalala.Ambaye amesema
“Wamejifunza mbinu za kuwasaidia vijana kuwa na ujasiri, uwezo wa kuchambua mambo, na kuishi kwa kujiamini hata katika mazingira magumu,”.

Kamishina wa Scout mkyoa wa Rukwa, Hassan Kikoloma, aliwapongeza wahitimu hao 20 kutoka shule mbalimbali za sekondari na kuwataka wazazi, walimu, na jamii kwa ujumla kushirikiana kwa karibu katika kuhamasisha watoto kujiunga na shughuli za Scout.

“Scout si tu kuvaa sare na kuimba nyimbo, ni mfumo wa maisha unaojenga viongozi wa kesho. Mafanikio ya vijana hawa yatategemea jinsi jamii inavyowapa nafasi na msaada,” amesema Kikoloma.

Katika dunia inayobadilika kwa kasi, kuwa na vijana wenye ujuzi wa vitendo, maadili, na uwezo wa kujitegemea ni hazina kubwa. Mafunzo ya Scout yana nafasi ya kipekee katika kulijenga taifa kupitia vijana wanaoandaliwa leo.