January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wahitimu TIA,watakiwa kutumia ufugaji samaki kujiajiri 

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza 

Wahitimu takribani 782, wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania(TIA),kampasi ya Mwanza wa ngazi mbalimbali,wametakiwa kubadili taaluma walioipata kuwa fursa ya kujiajiri kwa ajili ya maslahi yao binafsi,familia,jamii na taifa kwa ujumla.

Miongoni mwa fursa  ni pamoja na ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba ndani ya Ziwa Victoria, kwa kuchukua mikopo inayotolewa na Serikali kupitia Wizara ya Mifugo  na Uvuvi,kwa vijana kwa ajili ya ufugaji huo,ili kuondokana na changamoto ya ajira.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Alexander Mnyeti,

Hayo yameelezwa Novemba 29,2024 na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Alexander Mnyeti,wakati wa mahafali ya 22 ya TIA,ambayo yamefanyika kwa  mara ya pili kampasi ya Mwanza,iliopo Usagara wilayani Misungwi mkoani hapa.Amewatahadharisha wahitimu hao kuwa,wasidhani  huko nje,wao pekee ndio wasomi, hivyo lazima taaluma walioipata waitumie  kujiongeza na kutafuta fursa mbalimbali  ikiwemo ya ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba

“Nawasisitiza vijana wetu,Dunia imebadilika,msidhani huko nje kuna ajira zinawasubilia.Tatizo tulilonalo kwa wasomi wa taifa hili,wakiwa wanasoma chuoni wanahisi wao ndio wasomi pekee yao kuwahi kutokea katika nchi hii.Wanakuwa na matarajio makubwa,wakidhani huko uraiani kuna ajira, zinawasubilia wao waende wakapewe hizo nafasi,”amesema Mnyeti na kuongeza:

“Nimejulishwa kwamba TIA imewafundisha vijana kuajiriwa na kujiajiri,sasa hapo kwenye kujiajiri ndio mpigie mstari vizuri,ili mkitoka huko nje,mkajiajiri,”.

 Ameeleza katika kulitizama jambo la kujiajiri, Serikali imefungua milango kwa wasomi na wasio wasomi,ambapo kwa wasomi inawategemea kuwasaidia ambao hawajasoma katika kuwaongoza kwenye namna sahihi ya kujikwamua kiuchumi.

Hivyo Wizara ya Mifugo na Uvuvi,imepewa fedha na Serikali  zaidi ya bilioni 100,ambazo zinatumika kutengeneza vizimba vya ufugaji wa kisasa wa samaki Ziwa Victoria kwa ajili ya kuwawezesha vijana.

“Nyinyi wasomi wa leo,ili msifungamane  kusubili ajira,tunawapeni mikopo isiyo na riba.Tunakutengenezea vizimba tunakupa,unaweza kuchukua vitano mwingine vinne,pia unaweza kuchukua wewe mwenyewe au mkaungana na rafiki yako mkawa wawili hata watatu,mkachukua vizimba 20, mkafuga samaki,baada ya miezi nane mnaanza kuzalisha samaki,”.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa TIA Profesa William Pallangyo

Sanjari na hayo,Mnyeti,amesema Serikali inatoa kipaumbele kwa maendeleo ya elimu,na kwa kudhihirisha hilo kupitia mradi wa mageuzi ya kiuchumi kwa elimu ya juu,wanajenga mabweni ya wanafunzi katika  kampasi ya TIA Mwanza,yenye thamani ya bilioni 7.2.

“Leo tunashuhudia ongezeko la wahitimu kutoka 279 mwaka 2013 hadi kufikia 782 mwaka 2024,hivyo wahitimu 4,756,tayari wameishahiyimu masomo,na wanaendelea kulitumikia taifa katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Baadhi ya wahitimu wa TIA kampasi ya Mwanza,akiwemo Francis Haule,amesema fursa mtaani zipo nyingi zitakazowasaidia kujiajiri, ikiwemo ya ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba,hivyo atatumia fursa ya mkopo inayotolewa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kujiajiri.

Huku Sophia Abeid, amesema fursa ya vijana kujiunga vikundi au mmoja mmoja kwenda kupata mkopo kwa ajili ya ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba ni kitu kizuri kwao wahitimu kwani hawategemei kwenda kuajiriwa kwani kujiajiri ni kitu kizuri na wapo tayari.

Awali Ofisa Mtendaji Mkuu wa TIA Profesa William Pallangyo,amesema jumla ya wahitimu 782 wa kampasi ya Mwanza mwaka 2024,wamehitimu masomo yao katika ngazi mbalimbali,kati yao wanaume 397  sawa na asilimia 51 huku wanawake wakiwa  385 sawa na asilimia 49,”.

Ambapo amesema TIA kampasi ya Mwanza ilipokea kiasi cha bilioni 15, zikiwemo bilioni 7.8 zilizotumika kujenga  majengo  ya chuo hicho yaliozinduliwa Leo,ambayo yamepunguzia taasisi hiyo gharama za kukodisha majengo na kuchochea ufanisi.

“Jengo la chuo lina jumla ya madarasa Saba lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 1900, kwa wakati mmoja,maabara ya kisasa ina uwezo wa kuhudumia wanachuo 250,na maabara ya kompyuta ya kisasa yenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 200 kwa wakati mmoja, sambamba na ofisi 21 kwa ajili ya watumishi,”.

Baadhi ya wahitimu wa TIA kampasi ya Mwanza

Huku bilioni 7.2,zinazotokana na mradi wa mageuzi ya kiuchumi  kwa vyuo vya elimu ya juu, zinatumika kujenga hostel(mabweni), yatakayochukua wanafunzi wa kike 203 na wa kiume 103.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Johari Samizi,ametoa wito kwa wananchi wa maeneo hayo, kutumia fursa ya uwepo chuo hicho kuwekeza katika kujenga mabweni na kutoa huduma ya chakula, ili kuwasaidia wanafunzi hao kupata huduma hizo karibu na kuacha kutembea umbali mrefu.

Baadhi ya wahitimu wa TIA kampasi ya Mwanza