November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema

Wagonjwa wa Corona wazusha taharuki

Na David John

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema amethibitisha kujitokeza kwa taharuki katika Hospitali ya Amana, jijini Dar es Salaam iliyosababishwa na wagonjwa wa Corona waliopo hospitalini hapo kushinikiza warejee majumbani kwao kwa kile walichodai afya zao ziko poa (vizuri).

DC Mjema alitoa ufafanuzi huo jana wakati akizungumza na chombo kimoja cha habari (Sio Majira) pale alipoombwa na chombo hicho kueleza kinaendelea katika Hospitali ya Amana. Alisema ni kweli palitokea hali hiyo ya sintofahamu kwa baadhi ya wagonjwa kushinikiza kuondoka majumbani kwao kwa madai kwamba afya zao ziko poa.

Alisema baadhi ya wagonjwa walidai wapo hospitali hapo, huku wakiwa hawasikii maumivu wala chochote, hivyo ni bora warudi majumbani, jambo ambalo alisema sio sahihi.

“Nachotaka kusema hapa ni kwamba wagonjwa wetu wawe watulivu na kikubwa kuwasikiliza watalaamu wetu na kama miongoni mwao wataonekana kuwa wamepona watapata nafasi ya kuruhusiwa, hivyo ni vema tufuate maelekezo ya watalaamu,”alisisitiza.

Alipoulizwa kuhusu wagonjwa wanaodaiwa kutoroka hospitalini hapo, DC Mjema alisema watafuatilia kwa askari wanaolinda hospitali  kuona kama kuna wagonjwa wametoroka.

“Kitu kikubwa ni wagonjwa watulie tu huku watalaamu wakiendelea kuangalia afya zao na hakuna shaka wataruhusiwa tu endapo watabainika hawana changamoto yoyote,” alisema DC Mjema.

Taharuki hiyo ilijitokeza jana baada ya baadhi ya wagonjwa wa  Corona wanaopatiwa matibababu kuanza kushinikiza waruhusiwe waondoke waweze kurudi majumbani kwao.

Taarifa za wagonjwa kushinikiza waruhusiwe zilienea jana kwenye mitandao ya kijamii tangu asubuhi na kwamba walinzi wa hospitali hiyo kutoka Suma JKT walifanyakazi kubwa ya ziada kuwatuliza.

Inadaiwa wagonjwa hao walikuwa na hoja mbili, moja wakidai tangu wafike hospitali hapo huduma za dawa ni hafifu na pili wanadai  huduma ya chakula ni duni.

Mmoja wa wagonjwa (bila kutaja jina lake) alisema walifanya hivyo sio kwa nia ya kutoroka, bali kuweza kupaza sauti waweze kuboreshewa huduma. Alisema kuna mmoja wa wagonjwa alifariki, lakini mwili wake haukutolewa wodini, kwa hiyo wakasema hiyo haiwezekani, wakautoa wakitaka kuwapelekea hadi ofisini watoa huduma, huku wakipiga kelele zilizosikika nje.

“Kwa hiyo tukasema kwamba twendeni nje tukapaze sauti ili jamii ijue kinachoendelea, hivyo sio kweli kwamba watu wamekimbia, bali tulikuwa getini, baadaye tukashauriana turudi ndani, kwani tukienda huko nje tunaweza kusababisha madhara makubwa kwa jamii ambayo haikuwa na maambukizi,”alisema

Wakati huo huo, Serikali imewataka wahudumu wa afya nchini kufuata kanuni na miongozo iliyopo katika kutoa huduma kwa wagonjwa kwa kufanya hivyo wataweza kuepuka kupata maambukizi kutoka kwa wagonjwa wanaowahudumia.

Rai hiyo imetolewa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakati akipokea msaada wa vifaa vya kunawia mikono 100 vyenye ujazo wa lita 500 kutoka kwa Shirika lisilo la kiserikali la Water Mission Tanzania.

Waziri Ummy alisema kama mtaalamu wa afya atafuata mwongozo wa kuzuia maambukizi wa mwaka 2018  na muongozo wa uzuiaji wa maambukizi ya Virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Corona (COVID-19) wa mwezi wa kwanza mwaka 2020 hataweza kupata maambukizi kutoka kwa mgonjwa .

“Wakati tunaendelea kukabiliana na janga la ugonjwa wa COVID -19 tukumbuke kuwa kuna magonjwa mengine kama ya moyo, kisukari, maralia, figo na ya kuambukiza ikiwemo Ukimwi na kifua kikuu.

Hivyo basi mgonjwa wa aina hii akifika katika kituo cha kutolea huduma za  afya anatakiwa kutibiwa na siyo kukimbiwa,”alisema.

“Baadhi ya wahudumu wakimpokea mgonjwa mwenye joto kali wanamkimbia kwa kudhani kuwa ana ugonjwa unaosababishwa na virusi vya Corona. Mwongozo wa utoaji wa huduma za afya hauwataki kuwakimbia wagonjwa jambo la muhimu ni kufuata miongozo iliyopo hii ikiwa ni pamoja na kunawa mikono, kuvaa barakoa na glovu wakati una muhudumia mgonjwa ”, alisisitiza Waziri Ummy.

Aidha, Waziri Ummy alishukuru kwa msaada uliotolewa na Shirika hilo na kuwataka wananchi kuzingatia maagizo wanayopewa na wataalamu wa afya ikiwa ni pamoja na kunawa mikono kwa maji safi yanayotiririka na sabuni pamoja na kuvaa barakoa katika kukabiliana na ugonjwa wa Corona.