Na Heckton Chuwa,TimesMajira Oline,Moshi
ZAIDI ya wagonjwa 1,900 wamepatiwa huduma ya tiba shufaa katika hospitali ya rufaa ya Kanda ya KCMC, iliyoko Moshi, mkoani Kilimanjaro tangu kuanzishwa kwa huduma hiyo mwaka 2007, kupitia kitengo cha tiba ya saratani kilichoko, hospitalini hapo.
Tiba shufaa ni ile aambayo inayolenga kuboresha zaidi maisha ya watu walioathiriwa na magonjwa ambayo hayawezi kutibika, kwa njia ya kuzuia na kutuliza maumivi na mateso wanayoyapata kutokana na maumivu hayo.
Hayo yalielezwa na mratibu wa tiba shufaa katika kitengo hicho, Anna Massawe wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na tiba hiyo kuelekea maadhimisho ya kimataifa ya tiba shufaa yanayotarajiwa kufanyika hospitalini hapo Oktoba 10, mwaka huu.
“Wagonjwa hao walipatiwa tiba shufaa kwa kupatiwa dawa za kupunguza maumivu aina ya morphine pamoja na dawa nyingine zinazohusiana na tiba hiyo; hili limekua faraja kubwa kwa wagonjwa husika pamoja na jamaa zao,” alisema.
Alisema, wagonjwa waliopewa tiba hiyo ni wale ambao walikuwa wanaugua ugonjwa wa saratani iliyofikia hatua ya tatu na nne, wagonjwa wa Ukimwi waliofikia hatua ya mwisho pamoja na wale wenye ugonjwa wa kisukari ambao umeleta madhara kwa figo na macho kwa wagonjwa husika.
“Asilimia 60 ya wagonjwa wanaohitaji tiba shufaa hupendelea kupata tiba wawapo majumbani mwao kutokana ukweli kuwa huwa hawawezi hata kuinuka vitandani,”alisema.
Aidha, alisema tiba shufaa majumbani pia imekuwa msaada kwa wale ambao hawawezi kumudu gharama za kufuatilia tiba hizo kutokana na umbali wa kuzifuata hospitalini hapo ambapo uongozi wa hospitali huchukua jukumu la kuwahudimia wakiwa majumbani mwao.
“KCMC hotoea huduma hii bure kutokana na ufadhili uliotolewa na wamishonari kutoka nchini Ujerumani na hii imekuwa faraka kubwa kwa wagonjwa wengi wanaohitaji huduma ya tiba shufaa,”alisema.
Massawe aliendelea kusema kuwa, katika kupanua wigo wa huduma hiyo, hospitali ya KCMC imetoa msaada wa vifaa vya tiba shufaa kwa hospitali nne za Kibosho na Marangu zilizoko Moshi Vijijini, hospitali ya Machame iliyoko wilaya ya Hai pamoja na hospitali ya Huruma iliyoko wilayani Rombo.
“Pia tumeweza kutoa elimu ya tiba shufaa kwa maofisa afya zaidi ya 300 pamoja na maofisa wahudumu wa kujitolea ndani ya jamii zaidi ya 200 pamoja na baadhi ya ndugu na jamaa za wale ambao wanahitaji huduma hizo, ili waweze kuwahudumia wenyewe wawapo majumbani mwao,”aliongeza Massawe.
Kuhusu maadhimisho hayo ambayo hufanyika kila Jumamosi ya pili ya mwezi Oktoba ya kila mwaka,Massawe, alisema maofisa wa hospitali hiyo watatoe elimu kuhusiana na tiba hiyo kwa washiriki wa maadhimisho hayo na pia kupitia vyombo mbalimbali vya habari.
More Stories
Muhoji Sekondari kumaliza changamoto ya umbali kwa wanafunzi Musoma vijijini
Tanzania mwenyeji mkutano wa nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika
TANESCO yarudisha shukrani kwa jamii