November 15, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mgombea wa CCM, Dkt. John Maguguli.

Wagombea ubunge Kigoma wataka Magufuli apewe kura za kishindo

Na Penina Malundo,TimesMajira,Online

WABUNGE wa Mkoa wa Kigoma wampingia chapuo Rais John Magufuli kwa kuwataka wananchi wa mkoa huo kumpigia kura za kishindo ili aweze kumalizia awamu yake ya tano.

Rais Magufuli ni mgombea urais kwa tiketi ya CCM katika uchagu mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28, mwaka huu akichuana na wagombea wengine wa vyama vya upinzani.

Wamesema kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita amefanya mambo mbalimbali makubwa, ikiwemo uunganishaji wa barabara kutoka eneo moja kwenda lingine, elimu bure kwa shule za msingi na Sekondari, ujenzi wa vituo vya afya, hospitali pamoja na kuunganisha umeme katika majimbo ya wagombea ubunge hao.

Wagombea ubunge hao wametoa rai hiyo leo kwa nyakati tofauti kwenye mkutano ya kampeni wa Rais Magufuli. Wamesema Rais Magufuli amefanya vitu vingi vyenye tija, ambavyo vimeleta maendeleo katika nchi na kufanya nchi kuingia katika uchumi wa kati.

Akiomba kura leo katika Viwanja vya Lake Tanganyika katika mkutano wa Mgombea urais Dkt.Magufuli, Mgombea Ubunge wa Jimbo la Kasulu Mjini, Prof.Joyce Ndalichako, amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita amefanya kazi ya kutukuka, hivyo wananchi wampe kura kwa kishindo ili amalizie ahadi zake.

Amesema amefanya kazi kubwa hususani katika upande wa elimu na kwa kufanya elimu kuwa bure kumekuwepo kwa ongezeko la wanafunzi waliojiunga shule za msingi na Sekondari kwa mwaka huo.

“Kwa huku Kigoma, Serikali imeweza kujenga shule ya msingi na sekondari,vyuo vya ufundi kwa baadhi ya wilaya,ujenzi wa hosteli nchi nzima zaidi ya 600, maktaba za kisasa kwa lengo la kutoa huduma kwa wananchi,”amesema Prof, Ndalichako na kuongeza;

“Rais Magufuli amefanya mengi,ameonesha unyenyekevu mkubwa katika kuhakikisha nchi inakuwa na maendeleo.”

Aidha amesema kwa wilaya ya Kasulu, barabara kilometa 260 imejengwa kutoka Kibingo hadi Manyovu. Naye Mgombea Ubunge wa Jimbo la Buhingwe, Dkt.Philipo Mpango amesema yote yanayofanyika nchini ni kutokana n uchumi imara uliopo.

“Rais Magufuli ametutuma sisi wabunge watatu wa mkoa huu kumsaidia kazi naomba tumpe kura Rais wetu kwa asilimia 100 na sisi wabunge pamoja na madiwani,”amesema.