December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wagombea CHADEMA wakipewa ridhaa,watakuwa wawazi

Ashura Jumapili TimesMajira Online Kagera,

Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA), Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba,mkoani Kagera,kimesema,wagombea wao katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa wakipewa ridhaa,watakuwa wawazi na wakweli katika shughuli  za kimaendeleo,kufanya mikutano ya hadhara kila baada ya miezi mitatu ili kuwasomea Wananchi mapato na matumizi.

Huku kikiwahimiza,wananchi Novemba 27,2024, kujitokeza kupiga kura kwani ni haki yao kilatiba hata kama mgombea aliyekuwa anamtaka jina lake kukatwa.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa CHADEMA, Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba,mkoani Kagera Chief Kalumna. Novemba 21 2024,wakati wa uzinduzi rasmi wa kampeini wa chama hicho,katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa,ambapo amewanadi jumla ya wagombea 372 wakiwemo Wenyeviti,wajumbe wa makundi mchanganyiko na wanawake.

Kalumna,amesema kila baada ya miezi mitatu kwa mujibu wa sheria na kanuni zinazoongoza Halmashauri za Serikali za Mitaa ya mwaka 1984 na marekebisho yake, Wenyeviti wa Mitaa,Vijiji na Vitongoji wanatakiwa kufanya mikutano ya hadhara, na kuwasomea Wananchi mapato na matumizi ya maeneo yao,kusikiliza na kuzitatua kero za Wananchi ili kuleta amani kwa wakazi wa maeneo husika.

“Chama chetu, kitaendelea kuweka ukweli na uwazi kwa wananchi shughuli zote za kimaendeleo,hivyo wagombea wetu wakipewa  ridhaa ya kuwatumikia  katika uchaguzi huu, kila baada ya miezi mitatu watakuwa wanafanya mikutano ya hadhara na kuwasomea wananchi mapato na matumizi ya mitaa yao ili kuleta ufanisi wa kiutendaji,”.

Naye Katibu wa Baraza la Vijana CHADEMA (BAVICHA),Kanda ya Victoria Aron Ishengoma,ambaye ni mgombea uwenyekiti mtaa wa Pepsi amesema,chama hicho  kilisimamisha wagombea kila mtaa lakini wameondolewa na wengine majina yao kukatwa bila sababu za msingi.

Ishengoma,amesema kwa mujibu wa kanuni ya  35 kifungu cha 4,ya uchaguzi inasema bila kuathiri masharti ya kanuni ndogo ya tatu endapo kutakuwa na mgombea mmoja  wa nafasi ya Mwenyekiti wa Kijiji,Kitongoji na mtaa,makundi mchanganyiko au makundi ya wanawake unaruhusiwa kupiga kura ya ndiyo au hapana.

“Wananchi msiache kwenda kupiga kura kwa sababu wagombea wako wamekatwa badala yake jitokeze kwa wingi siku ya kupiga kura Novemba 27 mwaka huu kutimiza haki yenu ya kikatiba kwa kupiga kura ya hapana,”.