December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waganga wakuu waelekezwa kuboresha usimamizi wa utendaji huduma

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

NAIBU WAZIRI wa Afya Dkt. Godwin Mollel amewaelekeza Waganga Wakuu wa Mikoa kuboresha usismamizi wa utoaji wa huduma za afya katika vituo vya kutolea huduma wanavyosimamia nchini.

Dkt. Mollel ametoa rai hiyo leo Novemba 30, 2022 wakati akifunga Mkutano wa Waganga Wakuu wa Mikoa na Waratibu wa Mikoa wanaosimamia Masuala ya Ukimwi nchini uliofanyika siku moja kabla kuelekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani.

“Tanzania imepiga hatua kubwa kuboresha huduma za afya, lakini juhudi za ziada zinahitajika kuboresha zaidi ubora wa huduma tunazotoa, hivyo natoa rai kwenu kwenda kusimamia hilo ” amesema Dkt. Mollel.

Sambamba na hilo Dkt. Mollel amesema kuwa, wakati huu ambapo Serikali inalenga kwenda kwenye Bima ya Afya kwa wote ni vyema kwa watendaji katika vituo vya kutolea huduma za afya vya umma kuboresha zaidi huduma wanazotoa.

Kuhusu mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Virusi Vya Ukimwi, Dkt. Mollel amewapongeza watendaji pamoja na wadau wa Sekta ya Afya kusimamia vyema utekelezaji wa afua za mapambano dhidi ya Ukimwi na kuiewezesha Tanzania kupunguza kiwango cha maambukizi ya VVU kwa asilimia 62 toka mwaka 2010.

Aidha, Dkt. Mollel amewataka viongozi na watumishi kwa pamoja kuwajibika ipasavyo katika utoaji wa huduma bora ili kuweza kuokoa maisha ya Watanzania na kuwa na wananchi wenye afya njema wanaowajibika katika ujenzi wa nchi.

Sambamba na hilo ameendelea kusisitiza juu ya usimamizi mzuri wa dawa na kuhakikisha upungufu wa dawa haujitokezi katika vituo vyote vya kutolea huduma ili wananchi wasipate changamoto yoyote pindi wanapoenda kutafuta mahitaji.