November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waganda kipimo kizuri cha uwezo wa Ngorongoro Heroes

Na Philemon Muhanuzi,TimesMajira Online

TIMU ya vijana chini ya umri wa miaka 20 imefanikiwa kutinga hatua za fainali ya michuano ya afrika ikiwakilisha ukanda huu wa CECAFA pamoja na Uganda.

Haya ni mafanikio mengine kwa uongozi wa TFF unaoongozwa na Wallace Karia. Vijana wetu wanakwenda kukutana na vijana wa mataifa mengine na huko watacheza mechi zitakazowapa uzoefu mkubwa.

Kumfunga Djibouti magoli 6-1 au Somalia magoli 8-1 hakutoshi kuwapatia wachezaji aina ya uzoefu mgumu wenye kuweza kuwajenga kimpira. Mechi ya fainali ya michuano hii iliyofanyika mkoani Arusha timu yetu ikafungwa na Waganda magoli 4-1.

Na hiyo ndio ikawa mechi yenye kuweza kuwaonyesha makocha wa timu hii ni kipi wachezaji wetu wanakwenda kukutana nacho huko katika hizo mechi ngumu za makundi ya fainali.

Vijana wa Kisomali hawana uwezo wa kuonyesha udhaifu wa vijana wetu, wanapokutana kwa upande wa Ngorongoro Heroes ni kama wanakuwa mazoezini tu. Kelvin John na wenzake wanakuwa wakiteleza tu kuelekea golini.

Wanachagua ni dakika ipi wafunge na ipi wapasiane zile pasi za katikati ya uwanja. Vijana wa Uganda siku zote wanatusumbua kama timu ya wakubwa inavyowasumbua Taifa Stars.

Waganda wanautumia ujana wao ipasavyo. Wanacheza kwa nguvu na kwa kujituma. Wanacheza kwa ushirikiano, kila mmoja anacheza kwa kumsaidia mwenzake.

Wao wanaonekana kabisa kuwa ni timu moja, hakuna ile tabia ya mchezaji mmoja kucheza kiubinafsi akitafuta sifa kwa wale wanaomtazama pembeni ya uwanja.

Pia Waganda wamebarikiwa vimo na miili yenye kutazamika. Wengi wao ni warefu na wepesi wa maamuzi wakiwa na mpira na hata wasipokuwa nao. Wanalazimisha kupita na mpira katika mazingira magumu.

Mchezaji anaona kabisa mbele yake wapo vijana wawili wa Ngorongoro Heroes lakini anaamua kulazimisha kupita na mpira kuelekea mbele na sio kuingiwa na uoga na kuamua kupiga pasi za pembeni zisizo na madhara.

Tunalo tatizo la makipa, na hili ni matumaini kuwa makocha wameweza kuliona na wanajipanga kwa ajili ya kulitafutia ufumbuzi. Goli la kwanza walilofungwa vijana wetu ni la kizembe, kipa alitakiwa aupangue mpira wa adhabu kuliko kulazimisha kuudaka.

Mpira unaopigwa ukaelekea golini ukiwa unazunguka kwa kasi ni vigumu kwa kipa kuudaka, alitakiwa aupangie kuelekea kushoto kwake ili mabeki waliokuwa wamejipanga kutengeneza ukuta waweze kuuhamisha.

Goli la nne pia ni la kizembe kwa kipa aliyekuwa ameingia kuchukua nafasi ya mwenzake. Kipa anatakiwa asimame karibu na mstari wa goli pasipo kudanganyika kwamba mpira upo nusu ya pili ya uwanja. Kwa ufupi wake ilikuwa ni vigumu kuweza kuucheza mpira uliodunda mbele yake.

Lipo goli la mpira wa kona, wachezaji wa Uganda waliruka peke yao na mmojawao akafungwa pasipo kubughudhiwa na wachezaji wetu.

Labda tunaweza kusema kwamba Ngorongoro Heroes walisharidhika na kufanikiwa kuingia fainali za michuano ya Afrika chini ya miaka 20 hivyo mechi ya fainali waliicheza pasipo kutumia nguvu ya ziada.

Lakini mgeni wa heshima alikuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa. Ilikuwa ni hali ya fedheha kuwaona mashabiki wachache wa Uganda wakitamba na bendera zao halafu kamera ikielekezwa kwa mgeni wa heshima, anaonekana hafurahishwi na kile kinachoendelea uwanjani.

Huko katika hizo fainali tunakwenda kukutana na timu za mataifa yenye vijana wenye maumbo makubwa kama hawa Waganda na pengine kuwazidi. Vijana wa Senegal, Tunisia, Morocco au Cameroon ni wazi kwamba miili yao ni sawa na hii ya Waganda.

Kuanza kusema wenzetu hawa ni wakubwa kiumri kuliko wa kwetu ni mjadala mwingine wa kuendekeza ile tabia ya kujifariji. Hawa vijana wetu wamechaguliwa na makocha wazalendo wenye uzoefu wa miaka mingi wa kutazama uwezo wa mchezaji mmoja mmoja.

Hivyo lipo tatizo la udogo wa miili ya wachezaji wa miaka ya sasa. Hili tatizo hata Abdallah Kibaden Kocha mkongwe aliwahi kulielezea miaka mingi iliyopita.

Ngorongoro Heroes kwa kufungwa na vijana wa Uganda angalau wamecheza mechi inayowapa picha halisi ya nini wanakwenda kukutana nacho katika hizo fainali za Afrika.

Hongera ziwafikie viongozi wa TFF na makocha wanaofanya kazi kubwa ya kizalendo ya kuiinua Tanzania iweze kuonekana kimataifa.

%%%%%%%%%%%%%%%%%