*Washauria kutumia TVLA kwa ajili ya kupima wanyama kabla ya matibabu
*Wahimizwa kutumia chanjo za TVLA kudhibiti na kuzuia magonjwa ya mifugoÂ
Judith Ferdinand, Timesmajira Online -Mwanza
Wafugaji nchini na wadau wa mifugo wamehimizwa kutotibu mifugo yao kiholela bila kufuata utaratibu wa vipimo vya uhakika wa ugonjwa kabla ya kuanza matibabu kutoka Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania(TVLA).
Wito huo umetolewa Agosti 4,2025 na Daktari wa Mifugo Mtafiti Mkuu kutoka TVLA,Dkt.Ronald Benju, akizungumza na Timesmajira Online kwenye banda lao katika maonesho ya Wakulima Nane Nane,ambayo kwa Kanda ya Ziwa Magharibi yanafanyika Nyamh’onglo wilayani Ilemela mkoani Mwanza,yakiwa na kauli mbiu isemayo,”Chagua Viongozi Bora kwa maendeleo endelevu ya kilimo,mifugo na uvuvi 2025″.

Ambapo amesema,kupitia TVLA,wanyama watapimwa kisha wahusika watapewa sampuli ya matokea ya vipimo vya afya vya mifugo yao na kushauriwa dawa mahususi kwa ajili ya tiba.
Dkt.Benju,amesema,kwa miaka mingi kumekuwa na mazoea ya wafugaji kuwafanyia matibabu mifugo kiholela,hivyo wameshiriki katika maonesho hayo,ili kuwahamasisha na kuwaelimisha wananchi hususani wafugaji kwamba matibabu ya mifugo yanahitaji kufanyika baada ya vipimo.
Amesema kama ilivyo kwa binadamu na kwa wanyama pia ni muhimu kupima kwanza endapo mifugo inaonesha dalili za magonjwa na kutambua kwa usahihi ugonjwa upi unamsumbua kwani itasaidia kutumika dawa sahihi kutibu maradhi hayo.
“Athari ya utoaji tiba kwa mifugo kiholela bila kupitia maabara unaweza kuwapoteza.Kuwapatia dawa kunaweza kuwasababishia madhara ikiwemo kuugua zaidi au kufa kwa sababu hawana ugonjwa unaotakiwa kutibuwa na dawa hiyo.Kwanza mnyama anaumwa ukakosea ukampa dawa ambayo siyo sahihi unazidi kumuongezea msongo na usugu wa dawa,”amesisitiza Dkt Benju na kuongeza:
“Hivyo wakati utafika huyo mnyama wako atahitaji kutibuwa na dawa ambayo umeisha itumia vibaya awali itakuta wadudu wameisha kuwa sugu hivyo matiba yake kuwa magumu au yasifanikiwe,”.

Sanjari na hayo,Dkt Benju,amewashauri wafugaji na wadau wa mifugo, watumie chanjo za TVLA kwa ajili ya kuzuia na kudhibiti magonjwa ya wanyama na kuweka afya bora za mifugo yao na hatimaye kuwa na uzalishaji wenye tija.
Ambapo amesema,miongoni mwa jukumu la TVLA, ni pamoja na uzalishaji na usambazaji wa chanjo za mifugo na kwa sasa wanazalisha chanjo saba za magonjwa mbalimbali ya wanyama, ikiwemo chanjo ya mdondo au kideri kwa ajili ya ugonjwa wa kuku.
Pia chanjo kwa ajili ya ugonjwa wa chambavu kwa ng’ombe,chanjo ya kuzuia homa ya mapafu kwa ng’ombe kitaalamu ni CBPP,chanjo kwa ajili ya homa ya mapafu kwa mbuzi kitaalamu inatwa CCPP.
“Kadhalika chanjo ya kuzuia kutupa mimba na kitaalamu inatwa brucellosis,ambayo ni muhimu sana kwa sababu ni ugonjwa ambao unatoka kwa mnyama na kuingia kwa binadamu na ukiingia kwa binadamu unasababisha tatizo la afya kwa kiasi kikubwa,”amesema Dkt.Benju.


More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi