Judith Ferdinand, Maswa
Wilaya ya Maswa, mkoani Simiyu imemkumbusha Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega, ombi la kupatiwa eneo katika pori la kituo cha Shishiyu Holding Ground kwa ajili ya mradi wa unenepeshaji na uzalishaji wa malisho ya mifugo.
Akitoa taarifa kwa Naibu Waziri alipotembelea na kukagua shamba la mifugo la Shishiyu Holding Ground, Mkuu wa Wilaya ya Maswa Dkt.Seif Shekalaghe amesema,Wilaya hiyo mwaka 2017 iliandaa andiko maalum la kuomba kukabidhiwa kituo hicho kwa ajili ya unenepeshaji na uzalishaji wa malisho ya mifugo.
“Nia hiyo bado ipo na maandiko ya kutafuta wafadhili kugharamia shughuli hizo yako katika hatua nzuri, hivyo kwa mara nyingine tunaomba kutengewa ekari 1,500 kati ya ekari 10,240 za eneo lote la Shishiyu Holding Ground,” amesema Dkt. Shekalaghe.
Amesema,wakishatengewa eneo hilo litatumika kama moja ya shamba darasa kwa wafugaji haswa unenepeshaji mifugo, uzalishaji, utunzaji wa malisho ya mifugo, uanzishaji wa kituo cha kiini tete na uzalishaji wa mbegu bora za mbuzi na kondoo. Kwa upande wa wafugaji anaomba wapatiwe vitalu vya kuchungia mifugo kwa masharti yatakayowekwa na wizara.
Kwa sasa shughuli zinazofanyika katika kituo hicho ni wafugaji wa vijiji jirani kuchungia mifugo kwa kulipia ada ya malisho (grazing fee) ambayo ni shilingi 60 kwa mnyama mmoja kwa siku, ingawa vichaka vimepungua kwa kiasi kikubwa utoaji wa malisho ya mifugo huku miundombinu yake ikiwa chakavu ikiwemo nyumba za watumishi 6, majosho mawili,zizi la ng’ombe na bwawa moja lenye uwezo wa kuhifadhi maji lita za ujazo milioni 2.4 kwa mwaka.
Hata hivyo kwa sasa Wizara imeanza kufyeka vichaka kwa kutumia Gereza ya Malya ambapo lengo ni kufyeka ekari 100 kufikia Mei 31 mwaka huu lakini mpaka sasa jumla ya ekari 70 zimeisha fyekwa na shughuli zinaendelea.
More Stories
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari