Na Jumbe Ismailly, TimesMajira,Online, Igunga
WAFUGAJI wawili wa Kijiji cha Mwalala,Kata ya Nguvumoja,wilayani Igunga wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mfawidhi Wilaya ya Igunga wakikabiliwa na tuhuma za kuwazuia watoto wao kuendelea na masomo na kisha kuwaozesha kwa wanaume.
Wafugaji waliokamatwa na kufikishwa mahakamani ni Chai Mayanza(50) Salumu Kwitogwa (42) wote wakazi wa kijiji cha Mwalala kata ya Nguvumoja wilayani hapa.
Awali Mwendesha Mashtaka wa Polisi Wilaya ya Igunga, Alex Kataya alidai washtakiwa wote walitenda kosa hilo kinyume na kifungu 60 A(4) cha sheria ya elimu sura ya 350.
Mbele ya Hakimu wa Mahakama hiyo,Eddah Kahindi,Kataya alidai kwamba katika tarehe tofauti kati ya mwezi Januari na Augosti, mwaka huu,majira ya mchana katika Kijiji cha Mwalala, Kata ya Nguvumoja,wilaya ya Igunga na Mkoa wa Tabora washtakiwa walitenda kosa hilo.
Aidha Kataya alidai kwamba wafugaji hao wawili,wakiwa wazazi wa wanafunzi hao wenye umri wa miaka 16,waliwashawishi wanafunzi hao kuacha kuendelea na masomo ya sekondari katika shule ya Sekondari ya Nguvumoja na kuwaozesha.
Hata hivyo washtakiwa baada ya kusomewa shtaka hilo,walikana kutenda kosa hilo ambapo mshtakiwa Salumu Kwitogwa yupo nje kwa dhamana ya sh. milioni moja hadi Novemba 11, mwaka huu kesi hiyo itakapoanza kusikilizwa tena,kutokanana na upande wa mashtaka kudai upelelezi umekamilika.
Kwa mujibu wa mwendesha mashitaka huyo mshtakiwa wa pili,Chai Mayanza amepelekwa mahabusu hadi Oktoba 22,mwaka huu kutokana na kushindwa kutimiza masharti ya dhamana ya sh. milioni moja na mdhamini mmoja wa kueleweka.
More Stories
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi
Rais Samia apongezwa kwa kuboresha huduma kwa wazee
Watu 5,000 kuhudhuria tamasha la utamaduni Songea