January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wafanyakazi wa PURA washiriki sherehe za Mei Mosi

Na Mwandishi wetu,timesmajira,Online

WAFANYAKAZI wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) wameungana na maelfu ya Watanzania kufanya maandamano ya maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani jana yenye kauli mbiu isemayo mishahara na ‘maslahi bora kwa wafanyakazi ndiyo kilio chetu, kazi iendelee’.

Akizungumzia maadhimisho hayo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi PURA, Mhandisi Charles Sangweni amesema maadhimisho hayo ya Siku ya Wafanyakazi kwa mwaka huu ni ya sita kwa PURA kushiriki tangu kuanzishwa kwake mwaka 2015, na katika kipindi hiki imeshuhudiwa kasi ya kuimarika kwa taasisi hii ikiwa ni pamoja na ongezeko la watumishi na ufanisi katika utekelezaji wa shughuli za Mamlaka.

“Siku ya Mei Mosi ni muhimu kwetu watumishi wa PURA na watumishi wote duniani, kwani ni siku inayotukumbusha wajibu wetu wa kutumikia wananchi kwa uadilifu, kwa umoja, ufanisi na kwa haki inayostahili,” amesema.

Mhandishi Sangweni pia ametoa rai kwa wafanyakazi wa Mamlaka hiyo kuendelea na moyo wa kujituma na kuongeza ufanisi katika utendaji kazi ili kuleta matokeo chanya.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) kwa tawi la PURA, Abbas Kisuju amesema PURA imeungana na taasisi nyingine kwenye maandamano hayo ikiwa ni njia ya kutambua mchango wa watumishi kwenye utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka hiyo.

“Hii pia imekuwa fursa kwetu kuungana na wafanyakazi wa taasisi nyingine ili kubadilishana mawazo kuhusu utatuzi wa changamoto mbalimbali tunazokabiliana nazo kwenye maeneo yetu ya kazi,” ameongeza.

PURA imeshiriki kwenye maadhimisho hayo kwa wafanyakazi wa ofisi zake za Dar es Salaam na Dodoma kushiriki maadhimisho yaliyofanyika Dodoma.