May 11, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yajidhatiti kusomesha elimu ya juu wanafunzi watakafanya vizuri masomo ya sayansi

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

WAZIRI  wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda  amesema katika bajeti ya Mwaka wa Fedha 2022/23 Wizara imetenga fedha kwa ajili ya kutoa ufadhili wa masomo ya elimu ya juu  kwa wanafunzi watakaofanya vizuri katika masomo ya Sayansi kwa asilimia 100.

Mbali na hilo Prof.Mkenda  ametoa agizo kwa Bodi ya Mikopo nchini  kujipanga ili ifikapo mwaka wa fedha 2023/24 ianze  kutoa mikopo kwa wanafunzi watakaosoma masomo ya Ufundi na ujuzi kwa ngazi ya Diploma.

Akizungumza jijini hapa na  Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB)Prof.Mkenda alisema, wanafunzi hao wachache watakaofanya vizuri watasomeshwa ndani nan je ya nchi.

Aidha amesema,lengo la Serikali kutoa ufadhili

Huo ni kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu ya juu na kuhamasisha watoto wengi kupenda kusoma masomo ya Sayansi.

Kuhusu agizo kwa Bodi ya Mikopo kuangalia wanafunzi wanaosoma masomo ya Ufundi na Ujuzi kwa ngazi ya Diploma ,Waziri huyo amesema,katika eneo hilo  kuna ajira nyingi hivyo ni muhimu kutupia jicho wanafunzi wa masomo hayo.

“Sehemu ambayo ajira ni rahisi zaidi ni kwenye ufundi na ujuzi ambapo wengi wanaweza kujiajiri,hivyo ni vizuri kujiandaa…,na jambo hili  tunalisema mapema ili wanafunzi watakaoomba katika kipindi hicho wajue pia katika vyuo vya ufundi kuna fursa ya kupata mikopo,” amesema Prof. Mkenda

Ametumia nafasi hiyo kuwasihi wanafunzi wanaoomba mikopo ya elimu juu kutoa taarifa zote zinazotakiwa kwa ukamilifu na kwa wakati ili waweze kupata mikopo hiyo bila vikwazo wala  changamoto yoyote.

“Wanafunzi mnaoomba mikopo toeni taarifa zilizo sahihi,hii itawaepusha na changamoto ya kukosa mkopo maana kupata ama kukosa mkopo inategemea na taarifa zinazotolewa na mwombaji wa mkopo huo.”amesisitiza Prof.Mkenda

Mapema  Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Eliamani Sedoyeka amesema kwa sasa Wizara imejipanga kuhakikisha Watanzania wengi wanapata fursa ya kusoma elimu ya juu kwa kuwezesha kufanya hivyo kulingana na malengo ya Taifa letu.

Kwa upande wake  Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, Prof. Hamisi Dihenga amesema anatambua kuwa wana dhamana kubwa ya kuhakikisha utaratibu wa kutoa mikopo unaeleweka kwa Watanzania wote na unawasaidia wale wanaostahili kupata mikopo na kuahidi kushirikiana na Menejimenti ya Bodi ya Mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu kuhakikisha hilo linafanikiwa.