November 30, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wafanyakazi wa Benki ya NMB wapeperusha Bendera ya NMB Mlima Kilimanjaro

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Wafanyakazi 6 wa Benki ya NMB wamefanikiwa kupanda na kupeperusha bendera ya NMB katika kilele cha Mlima Kilimanjaro kama sehemu ya kuadhimisha Mwezi wa Huduma kwa Wateja, unaoadhimishwa duniani kote kila Oktoba.
 
Benki hiyo pia, imelitumia tukio hili la kihistoria kama sehemu ya kuwahamasisha wafanyakazi wake na Watazania kwa ujumla kushiriki utalii wa ndani ili kusaidia kukua kwa shughuli hiyo yenye fursa lukuki kibiashra na tija kiuchumi.

Tukio la kusherekea Mwezi wa Huduma kwa Wateja mita 5,895 juu ya usawa wa bahari, umekua na maana kubwa kwa namna benki hiyo inavyozingatia huduma bora kwa wateja wake na kuudhihirishia umma kuwa ni kinara wa kutoa masuluhisho mbali mbali kwa wateja wake, ikiwemo kuwawezesha kuteleza kidijitali mahali popole na wakati wowote kupitia NMB Mkononi (Piga 150 66# au App), Lipa Mkononi (QR) na NMB Direct.

Timu hiyo ya NMB imetumia siku saba kupanda na kushuka Mlima Kilimanjaro wakianzia lango la Machame na kumalizia lango la Mweka, walipokelewa na wenzao kutoka ofisi ya Kanda ya Kaskazini pamoja na matawi ya Moshi.

Aidha, hiki kimekuwa ni kitendo cha kutambua umuhimu wa biashara ya utalii na jukumu la msingi kwa sekta hiyo katika uchumi wa taifa na maendeleo ya nchi kwa ujumla.
 
Akizungumza wakati wa kuwapokea wafanyakazi hao kutoka mlimani, Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro – Bw. Iman Kikoti alisema kuwa, kitendo cha wafanyakazi wa NMB kupanda Mlima Kilimanjaro kinaimarisha nafasi ya benki hiyo kuendelea kuwa karibu na sekta ya utalii na mshirika wa kimkakati wa maendeleo ya taifa.
 
Pia alibainisha kuwa, uamuzi wa NMB wa kuhamasisha utalii wa ndani ni kielekezo cha utayari wake kuchangia maendeleo na ustawi wa tasnia hiyo ili iweze kuchangia kikamilifu kuchochea kukua kwa uchumi nchini na ujenzi wa taifa.

Bw. Kikoti aliipongeza NMB kwa hilo huku akisisitiza kuwa utalii wa ndani ni hazina kubwa kwa taifa ambayo inahitaji ushirikiano wa wadau kuufanya kushamili na kuchangia kukua kwa sekta nzima ya utalii nchini.
 
“Kwa sasa mchango wa utalii bado ni mdogo kwa hiyo uamuzi wa NMB kusaidia kuuchangamsha ni jambo jema na la kimaendeleo linalopaswa kuungwa mkono na wadau wote wa sekta binafsi,” alibainisha.
 
Nae kiongozi wa safari hiyo ambaye ni Afisa Mkuu wa Wateja Wakubwa na Serikali wa Benki ya NMB, Bw. Alfred Shao, alisema kamwe hawatajutia kushiriki kwenye zoezi hilo lilowafunza mambo mengi ya kimaisha na kikazi.

Wafanyakazi wa Benki ya NMB pamoja na wasindikizaji wa wenzao waliopanda Mlima Kilimanjaro, wakiwashangilia wenzao waliopanda na kushuka Mlima huo kwa siku Saba, katika hafla ya mapokezi  iliyofanyika katika lango la Mweka.
Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro – Bw. Iman Kikoti katika picha ya pamoja na timu ya Wafanyakazi wa NMB waliopanda Mlima Kilimanjaro, baada ya kuwatunuku vyeti kuashiria walifika katika  kilele cha Mlima huo mrefu Afrika – Uhuru Peak
 Wafanyakazi wa Benki ya NMB wakiipeperusha bendera ya Benki hiyo yenye ujumbe ‘Huduma kwetu Shangwe’ wakiwa katika kilele cha Mlima Kilimanjaro, kama ishara ya kusherehekea huduma  wanazozitoa kwa wateja wao na jamii kwa ujumla.
Wafanyakazi wa Benki ya NMB  wakiipeperusha bendera ya Benki hiyo wakiwa katika kilele cha Mlima Kilimanjaro, kama ishara ya kusherehekea Mwezi wa Huduma kwa Wateja.