November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wafanyabiashara wapigwa marufuku kupanga bidhaa chini

Na Heri Shaaban, TimesMajira Online, Ilala

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Amos Makalla, amepiga marufuku wafanyabiashara kupanga Biashara za matunda na vyakula chini ni hatari kiafya msimu huu wa mvua ambapo kunaweza kutokea magonjwa ya mlipuko ikiwemo Kipindupindu.

Mkuu wa mkoa Makalla ametoa agizo hilo wakati wa zoezi la usafi wa pamoja soko la Machinga complex ambapo amewataka Viongozi wa masoko yote kudhibiti na kusimamia maelekezo hayo kwa ajili ya Tahadhari ya magonjwa ya kipindupindu .

Aidha Makalla aliwataka Viongozi wa masoko yote Mkoa Dar es Salaam kuwa wasafi masoko yao wakati wote Ili kulinda Afya za walaji wakati huu wa mvua za masika .

Katika hatua nyingine amesema wafanyabiashara waliokuwa soko la kariakoo kuwa ujenzi ukikamilika kipaombele kitakuwa kwa wale waliokuwepo awali kupewa maeneo ya biashara zao.

Aliwataka Wafanyabiashara kuzingatia kuheshimu maeneo yaliokatazwa ambayo yamepigwa marufuku ufanyaji biashara na kuwataka kwenda kwenye masoko rasmi Ili waweze kunufaika na fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali hususani mikopo.

Alitumia nafasi hiyo kumpongeza Meneja wa Soko la Machinga Complex Kwa usimamizi mzuri wa soko hilo ambalo limekuwa kivutio ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam .

Katibu Tawala Mkoa Dar es Salaam Rehema Madenge amewataka Watendaji wa Kata ,Mitaa na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa kila Jumamosi wanafanya Usafi katika maeneo yao.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo alisema usafi ni wetu sote sio jukumu la Serikali hivyo alitumia nafasi hiyo kuwataka wananchi wa Wilaya ya Ilala kuzingatia usafi katika maeneo yao wakati wote.