June 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wafanyabiashara wapewa elimu ya fedha

Na. Josephine Majula, WF-Kagera

MKUU wa Wilaya ya Bukoba Erasto Sima, amewataka watoa huduma za Fedha kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa na Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania wakati wa kutoa huduma za fedha kwa wananchi.

Agizo hilo amelitoa alipokutana na Timu ya wataalamu ya Wizara ya Fedha ambao wamefika mkoani Kagera kwa ajili ya kutoa elimu ya huduma za fedha kwa wananchi katika makundi mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara, wajasiriamali na wanafunzi.

“Watoa huduma ya fedha msifanye biashara kwa mazoea mfuate utaratibu uliowekwa na Serikali ukiwemo wa kupata leseni kwa mamlaka zinazotambulika kisheria kwa ajili ya kutoa huduma za fedha.”, amesema Sima. 

Kwa upande wake Afisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Bw. Stanley Kibakaya, amesema kuwa kutokana na wananchi wengi kutapeliwa wanapohitaji huduma za fedha, Wizara ya Fedha imeamua kutatua changamoto hiyo kwa kutoa elimu ya fedha kwa njia mbalimbali ikiwemo ya filamu.

Bw. Kibakaya amesema kuwa Timu ya wataalamu itatoa mafunzo hayo kupitia filamu iliyoandaliwa mahususi ikiwa na mada mbalimbali za elimu ya fedha ikiwemo uwekaji akiba, uwekezaji, kuweka mipango kwa ajili ya uzeeni, usimamizi binafsi wa fedha na mikopo.

Naye Mfanyabiashara Bi. Lilian Lugakingira aliishukuru Wizara ya Fedha kwa kuwafikia na kuwapa elimu hiyo muhimu kwa kuwa itawasaidia kuwa na uelewa mpana wa masuala ya fedha.

“Nimefurahi sana kupata elimu ya fedha, nimepata elimu nzuri ya namna bora ya kuweka akiba na kufanya uwekezaji kupitia faida nitakayoipata kwenye biashara yangu, nitawaelimisha wenzangu ili waweze pia kujiwekea akiba na kuwekeza katika Taasisi rasmi ili waweze kupata faida” alisema Bi. Lugakingira.

Katika kutoa elimu kwa wananchi kwenye mikoa hiyo Timu ya wataalamu wa Wizara ya Fedha imeambata na wataalamu kutoka Taasisi nyingine za Serikali ikiwemo Mamlaka ya Masoko na Mitaji na Dhamana (CMSA) na Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Wizara ya Fedha imeanza kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wa makundi mbalimbali katika mikoa nane ikiwemo Kagera, Singida, Manyara ikiwa ni utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha kwa mwaka 2021/2022 hadi 2029/2030.