January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wafanyabiashara waomba elimu ya namna watakavyorejea soko kuu

Judith Ferdinand, Mwanza

Halmashauri ya Jiji la Mwanza,imeombwa kutoa elimu na utaratibu kwa wafanyabiashara waliopisha ujenzi wa soko kuu kwa hiari yao namna watakavyo rejea sokoni hapo,pindi ujenzi wa soko hilo utakapo kamilika,ili waweze kufanya biashara na kuchangia pato la Taifa kwa kulipa kodi na tozo mbalimbali.

Kauli hiyo wameitoa baada ya agizo la Rais Samia Suluhu Hassan,alioitoa wakati akihutubia kwenye maadhimisho ya kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru,yaliofanyika jijini Mwanza,Oktoba 14,2024,ambapo aliuagiza Uongozi wa jiji la Mwanza kukamilisha ujenzi wa soko hilo kabla ifikapo Desemba, na kuhakikisha soko hilo linatumiwa na wanamwanza huku akisisitiza kutoa kipaumbele kwa wafanyabiashara waliokuewpo awali na wakapisha ujenzi wa soko hilo.

Wakizungumza jijini hapa na majira baadhi ya wafanyabiashara hao licha ya kumpongeza Raisi Samia kwa kutilia mkazo suala hilo wamesema bado Halimashauri ya Jiji la Mwanza,haijaweka wazi utaratibu wa kuwarejesha wafanyabiashara hao ndogo ndogo kwenye soko hilo hali inayowaacha njia panda.

Mmoja wa wafanyabiashara ndogo ndogo,jijini Mwanza Peter Fokolo, ameeleza kuwa tangu Rais atoe kauli hiyo,bado hawajapata maelekezo yoyote kutoka katika uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza,ambako kuna ofisi ya biashara na Maofisa masoko.

“Tulitegemea wangeyaita makundi ya wajasiriamali wadogo wadogo ambao sasa wanapanga kwenda kuwa wafanyabiashara wa kati,na kuwapa semina na elimu ya namna ya kuingia ndani soko kuu,kufanya biashara na vigezo gani vinatakiwa kutumika, lakini mpaka sasa hatujapata,”amesema Fokolo.

Rehema Mbise,mmoja wa wafanyabiashara ndogo ndogo waliopisha ujenzi wa soko hilo,ametoa wito kwa Halmashauri ya Jiji la Mwanza kutii,amri ya Rais Samia, ya kuwapa kipaumbele cha kuwapatia wao waliopisha mradi maeneo.

“Wafanyabiashara wengi hatujui tutaingiaje, wanasubili kwamba soko limekwisha basi kila mmoja ataingia.Zamani tulikuwa tunapata kitambulisho cha 20000, lakini sasa hivi tunajua tutaingia kwa tenda hivyo tupewe elimu kama mtu ataingia kwa tin namba au leseni ya biashara ili tutafute mapema,”amesema Rehema.