Na Lubango Mleka,Igunga
MKUU wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt Batilda Buriani amepiga marufuku na kuwaonya wafanyabiashara na wawekezaji wenye viwanda bubu vya kutengeneza mifuko ya Plastiki iliyopigwa marufuku nchini kuendelea kutengeneza.
Akizungumza katika maadhimisho ya kilele cha wiki ya mazingira Duniani yanayofanyika kila mwaka Juni 5, ambapo kwa mkoa wa Tabora yamefanyika wilaya ya Igunga katika viwanja vya Sabasaba Jana , amesema wananchi, wafanyabiashara ambao wana viwanda bubu vya kutengeneza mifuko ya Plastiki iliyopigwa marufuku na serikali kuacha kuitumia na kuzalisha mifuko hiyo kwani imeonekana kuwa chanzo kikubwa cha uchafuzi wa mazingira.
” Ndugu Wananchi siku ya mazingira Duniani ni siku ya umoja wa mataifa kuwaelimisha na kuwahimiza watu duniani kote kuchukua hatua katika kuyatunza na kulinda mazingira kwani nchi zina mipaka lakini mazingira hayana mipaka awareness and action to protect our environment. Napenda kuwakumbusha kaulimbiu ya siku ya Mazingira Duniani inayosema masuluhisho kwa uchafuzi wa plastiki au Komesha Uchafuzi wa Plastiki (Beat Plastic Pollution),” amesema Balozi Dkt Buriani.
Amesema kuwa, zaidi ya tani milioni 400 za plastiki huzalishwa kila mwaka hapa Duniani na nusu yake hutumika mara moja tu na kutupwa na ni kati ya hizo,asilimia 10 tu hurejelezwa tena kwa matumizi.
“Inakadiriwa kuwa tani milioni 19 hadi 23 huishia katika mito, maziwa na bahari, pia kufukiwa na mingine huchomwa moto na kutoa hewa yenye sumu, vipande vidogovigogo vya plastiki huweza kupenya kwenye vyakula tunavyokula, maji tunayokunywa na kwenye hewa tunayoivuta na kusababisha matatizo katika afya zetu,”amesema na kuongezaÂ
” Naomba tuadhimishe siku ya mazingira duniani kwa vitendo, tukifanya usafi na kuondoa taka zote ngumu na hasa za plastiki, tukitumia nishati mbadala mfano Solar na gesi, majiko banifu yanayotumia kuni na mkaa kidogo na kuwa na mpango kabambe wa hifadhi ya mazingira, sasa ni marufuku kwa viwanda bubu vinavyotengeneza mifuko ya plastiki katika mkoa wa Tabora, kwa yoyote atakayebainika kutengeneza, kutumia au kuingiza mifuko hii hatua kali za kisheria zitachukuliwa ikiwa ni kufikishwa Mahakamani au kupigwa faini,” amesema Balozi Dkt Buriani.
Kwa upande wake Afisa Mazingira Mkoa wa Tabora, Abrahaman Mdeme amesema kuwa, ongezeko la idadi ya watu katika mkoa wa Tabora kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012 mkoa wa Tabora ulikuwa na idadi ya wakazi 2,291,622 hii ni ongezeko la watu takribani 1,100,056 ndani ya miaka kumi 2021-2022 na linaenda sambamba na uharibifu wa mazingira unaosababibishwa na shughuli nyingi za kibinadamu.
” Taarifa na takwimu mbalimbali zilizofanyiwa utafiti zinaonesha kuwa kiwango cha ukataji wa misitu kwa mwaka nchini kinakadiriwa kuwa takribani hekta 372,816, kulingana na taarifa ya NAFORMA ya mwaka 2015 na pia makadirio ya karibuni ya mwaka 2018 kutoka kituo cha Taifa cha utafiti wa hewa ukaa (NCMC) yanaonesha uharibifu wa misitu kwa mwaka nchini umeongezeka na kufikia takribani hekta 469,420,” amesema Mdeme.
Amesema kuwa, uharibifu huo unatokana na mambo mbalimbali ikiwemo ukataji wa miti kwa ajili mbao, fito na nguzo kwa ajili ya ujenzi, kuni kwa ajili ya ukusanyaji wa tumbaku na kupikia majumbani, makaa kwa ajili ya kupikia na ufyekaji wa misitu kwa ajili ya upanuzi wa mashamba, maeneo ya makazi na maendeleo, haya yote ni mahitaji ya kibinadamu na ambayo yanaongezeka kwa jinsi wananchi wanavyoongezeka.
” Utafiti uliofanyika kubaini kasi ya uharibifu wa mazingira Magharibi mwa nchi katika mikoa ya Tabora, Kigoma, Katavi na Shinyanga kutoka ofisi ya Makamu wa Rais kati ya mwaka 2002 hadi 2013 unaonesha hekari 202,051 zinapotea kila mwaka, aidha utafiti huo unaonesha ukanda wa magharibi hasa mkoa wa Tabora unaongeza kwa kasi ya uharibifu wa misitu na mazingira, maeneo mengi ya wilaya za Igunga, Nzega yanaonekana dhahiri katika picha za anga kuwa yameathirika zaidi yakifuatiwa na wilaya ya uyui,” amesema Mdeme.
More Stories
RC Chalamila awataka ndugu,Jamaa na marafiki kuwa wavumilivu zoezi la uokoaji likiendelea
Baraza la Madiwani lafukuza watumishi wawili idara ya afya
Wanasheria waombwa kusaidia kusimamia sheria, sera ulinzi wa taarifa