January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waendesha shughuli za mgodi bila vyoo

Na Suleiman Abeid
Timesmajira Online, Shinyanga


MGODI mdogo wa dhahabu unaomilikiwa na wawekezaji wazawa Chapakazi Partners uliopo katika kijiji cha Wisolele Kata ya Segese wilayani Kahama mkoani Shinyanga umetajwa kuendesha shughuli zake pasipo kuwa na vyoo.


Hali hiyo imebainika wakati Mkoa wa Shinyanga hivi sasa ukiwa unakabiliwa na ugonjwa wa kipindupindu kwa baadhi ya Halmashauri zake hadi kufikia wiki iliyopita waliripotiwa wagonjwa 216 huku 127 wakibainika kuwa na ugonjwa huo.

Katibu wa Mgodi mdogo wa dhahabu wa Chapakazi Partners, Stephen Lutego.


Katika taarifa yake kwa wajumbe wa Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) mwishoni mwa wiki iliyopita, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme amewataka maofisa afya wote mkoani humo kuhakikisha wanasimamia suala la usafi wa mazingira ikiwemo uwepo wa vyoo na maji tiririka kwa ajili ya kunawa mikono.


Waandishi wa habari ambao wametembelea mgodi huo wa Chapakazi wameshuhudia kutokuwepo kwa huduma za vyoo katika maeneo yote ya mgodi ambapo baadhi ya viongozi wamedai vilivyokuwepo vimejaa na hivyo kulazimika kufungwa.


Mmoja wa wananchi katika eneo hilo kwa sharti la kutotajwa jina amesema changamoto ya ukosefu wa vyoo katika mgodi huo ni la kipindi kirefu na kwamba wengi wao hujisaidia vichakani jambo ambalo ni hatari kwa afya linaweza kusababisha mlipuko wa magonjwa ikiwemo kipindupindu.


“Tumesikia Mkoa wetu wa Shinyanga bado unakabiliwa na ugonjwa wa kipindupindu, sasa iwapo maambukizi yatafika kwenye maeneo haya ya machimbo ipo hatari ya watu wengi kukumbwa na ugonjwa huo ni vyema mamlaka husika zikaliona hili,” ameeleza mwananchi huyo.


Mbali ya kutokuwepo kwa vyoo pia mgodi huo umekuwa hauna utaratibu mzuri wa utiririshaji wa maji yanayotolewa kwenye mashimo (duara) ya machimbo ya dhahabu ambayo bomba lake limeelekezwa kwenya maeneo yenye makazi ya watu na shughuli za kijamii hali inayoweza kusababisha madhara iwapo yatakuwa na kemikali.


“Haya maji yanayotoka huko juu kwa kweli hatuelewi kama ni salama ama yana kemikali fulani, maana hakuna mtu ambaye ameyapima,wenzetu wanayaachia tu bila utaratibu mzuri, ni vyema yangefanyiwa utaribu wa kuchimbiwa mashimo badala ya kuachwa yasambae ovyo,” ameeleza Shija Charles mjasiriamali Wisolele.

Muonekano wa makazi ya wachimbaji wadogo wa dhahabu katika kijiji cha Wisolele kata ya Segese wilayani Kahama.


Edward Herman ambaye ni Msimamizi wa Usalama katika mgodi huo amesema tayari kuna utaratibu ambao unaendelea ikiwemo suala la ujenzi wa vyoo pamoja na utekelezaji wa maagizo ya Wizara ambayo imetolewa hivi karibuni.


“Kama mnavyoona hapa shughuli za kurekebisha maeneo yetu ya uchimbaji zinaendelea,tumesimamisha uzalishaji ili tuweze kukamilisha kazi hii. Juzi tulikuwa na wakaguzi kutoka Wizara ya Madini ambao wamekagua eneo letu, tunasubiri maelekezo yao,”ameeleza na kuongeza kuwa


“Siyo kwamba hatuna vyoo hapa, vilikuwepo lakini kwa sasa tumevifunga kwa vile vimejaa,tupo katika harakati za kutengeneza vyoo vingine, tunajitahidi ili tuweze kukamilisha,” ameeleza Herman.


Kwa upande wake Ofisa Madini Mkoa wa Kimadini Kahama, Joseph Kumburu amesema hivi sasa tayari kuna timu ya ufuatiliaji wa utekelezaji maelekezo yaliyotolewa na Wizara inapita migodini kufanya ukaguzi kwenye migodi yote iliyopo wilayani Kahama.

Bomba la maji ambayo usalama wake haufahamiki yakitiririka kutoka kwenye maduara ya dhahabu kuelekea maeneo ya chini ya mlima ambako kuna makazi ya watu wanaoendesha shughuli mbalimbali za kibinadamu