March 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wadau watakiwa kuelimisha jamii kuhusu programu Jumuishi ya MMMAM

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

WAKATI Serikali ikitekeleza Programu jumuishi ya Taifa ya Malezi ,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) ya miaka mitano 2021/22-2025/26,wadau nao wameombwa kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa programu hiyo kwa kuweka kwenye bajeti zao kwa lengo la kufikisha elimu hiyo katika jamii.

Asilimia 43 ya watoto nchini Tanzania wapo kwenye hatari ya kutofikia hatua timilifu za ukuaji na maendeleo kutokana na viashiria mbalimbali vya hatari vya maendeleo kama vile utapiamlo ,umasikini,kukosekana kwa uhakika wa chakula ,msongo wa kifamilia ,miundombinu duni na uhaba wa rasilimali pamoja na utekelezaji na unyanyasaji wa watoto.

Akifunga mafunzo kwa wadau yaliyoandaliwa na Mtandao wa Malezi,Makuzi (TECDEN) na kufanyika jijini Dodoma,Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Ofisi ya Rais ,Tawala za Mikoa na Seriakli za Mitaa (TAMISEMI) Shabani Muhali alisema,hatua hiyo itasaidia elimu ya malezi na makuzi kufika kwa jamii na hivyo kufanikisha lengo la Programu ya MMMAM na hatimaye kujenga kizazi chenye tija kwa Taifa.

Muhali ambaye aliiwakilisha TAMISEMI katika mafunzo hayo amesema,Serikali imeamua kuja na programu ya kuwaleta wadau pamoja katika kushughulikia masuala ya mtoto tangu akiwa tumboni ili kuhakikisha jamii inalea watoto kwa kuzingatia mambo yote muhimu yakiwemo Afya bora,lishe ya kutosha,malezi yenye mwitikio,ujifunzaji wa awali pamoja na ulizni na usalama wa mtoto huku akisema malezi hayo  humfanya mtoto kukua katika utimilifu wake.

Aidha kiongozi huyo ametumia nafasi hiyo kuwaongoza wadau hao kula kiapo cha kwenda kuifanya kazi ya kuelimisha jamii kuhusu Programu ya MMMAM ili kufika kwa jamii na siyo kubaki kwenye makabati.

Mkurugenzi wa TECDEN Mwajuma Rwebangira amesema inawategemea wadau hao kwamba wanakwenda kufanya kazi ya kuhakikisha PJT-MMMAM  inakwenda kufanikiwa katika utekelezaji wake.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Shirika la Malezi na Makuzi ya Mtoto (CiC) Craig Ferla alisema,wadau ni moja ya watu wanaotegemewa katika mafanikio ya utekelezaji wa Programu hiyo.

Mkurugenzi wa Shirika lilisilo la Kiserikali la Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (CiC) Craig Ferla akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa malezi na makuzi ya watoto jijini Dodoma

Aidha amesema Programu ya MMMAM ni fursa ya kipekee kwa Taifa ambayo inahitaji ushirikiano wa wadau kwa lengo la kuhakikisha mtoto anakuwa katika utimifu wake.

“Mwaka huu tuna zoezi la Sensa ya Watu na Makazi,Sintashangaa kuona theluthi moja ya watanzania kuwa ni watoto wadogo wenye umri kati ya miaka 0-8,kwa mantiki hiyo kama Taifa tukiweza kuwekeza kwa watoto hao ,tutakuwa na Taifa bora la kesho.”alisema Craig na kuongeza kuwa

“Katika maendeleo ya mtoto kila afua ina nafasi yake hivyo inahitaji ushirikiano wa wadau ili tupige hatua kufikia njozi za Taifa.,”

Kwa upande wadau nao waliahidi kufanya kazi ya kufikisha elimu kwa jamii kama walivyopata mafunzo huku kila mkoa ukiweka mpango kazi wake huku kwa upande wa Maafisa Ustawi na Maafisa Maendeleo ya Jamii wakiahidi ushirikiano kwa waandishi wa habari katika utekelezaji wa prograu hiyo .

Felista John Mwakilishi wa Taasisi za Kimataifa aliahidi kutoa ushirikiano katika jambo hilo kwa kadri itakavyohitaika.

Akizungumza na mtandao huu,Rehema Francis Mkazi wa Majengo jijini Dodoma amishukuru Serikali kuanzisha programu hiyo huku akiiomba Serikali na wadau wafanye kila linalowezekana kuhakikisha elimu ya malezi,makuzi na maendeleo ya awali inafika kwa jamii na kuiishi.

“Elimu hii ikifika kwa jamii ipasavyo itasaidia sana kuwalea watoto kwa kuzingatia maeneo muhimu ya ukuaji wao,nasema hivi kwa sababu wapo wakina mama ambao huwapiga sana watoto wao wadogo wasiokuwa hata na uwezo wa kusema ,lakini unakuta mama huyu anafanya hivyo bila kujua madhara anayomsababishia mtoto huyo.”amesema Rehema