March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wadau wapendekeza hatua kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa 2050

*Washiriki katika kongamano juu ya  nafasi ya ubia kufikia malengo ya Dira

*Wasisitiza tafiti kufanyika

*Kafulila aeleza umuhimu wa ubia kufikia malengo

Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza

Wadau mkoani Mwanza wameeleza hatua mbalimbali za kuchukuliwa ili kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ikiwa ni pamoja na Pato la Taifa kufikia dola tirioni moja.

Hayo yamebainishwa Julai 26,2025 na wadau hao katika Kongamano juu ya nafasi ya ubia katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,lililofanyika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agoustino (SAUT) jijini Mwanza, lililoandaliwa na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi(PPPC) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu  cha Dar-es-Salaam,Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (REDET).

Mkurugenzi wa PPPC,David Kafulila akizungumza katika kongamano juu ya nafasi ya ubia katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,lililofanyika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agoustino (SAUT) jijini Mwanza, lililoandaliwa na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi(PPPC) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu  cha Dar-es-Salaam,Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (REDET).

Akiwasilisha mada ya dhana ya PPP na nafasi yake kufikia Dira ya Taifa 2050, Mkurugenzi wa PPPC,David Kafulila,amesema Tanzania inalenga kuwa na pato la dola 7000 kwa kila mtanzania huku la Taifa kuwa dola tirioni  moja,kufikia mwaka 2050.

“Haya ni malengo makubwa lakini yanatekelezeka na ni wajibu wa kila mtu kushiriki ipasavyo ili kuyafikia.Kwa sasa zipo nchi 19 tu duniani zenye ukubwa wa uchumi huo ikiwemo Korea Kusini na Vietnam kama nchi ambazo zimefanya mageuzi makubwa ya kiuchumi kwa muda mfupi,amesema Kafulila na kuongeza:

“Tanzania imeweka mazingira bora ya sheria na sera ili kuimarisha nafasi ya ubia kwenye uchumi wa nchi na tayari matokeo ya awali yameanza kuonekana na yatakuwa wazi zaidi kwenye utekelezaji wa Dira,”.

Amesema Dira hiyo ni ya pili ikitanguliwa na ilioanza kipindi cha Rais wa awamu ya tatu Hayati Benjamin Mkapa, hivyo ili kuitekeleza lazima kufanyike uwekezaji mkubwa katika miradi ya maendeleo na kujenga uchumi mkubwa huku akihimiza utafiti juu ya ubia ili kusaidia kufikia malengo.

“Ni lazima sekta binafsi ichukue jukumu lake kwani sababu kubwa ya kufanya ubia nikusaidia serikali  kwa kukuza mitaji,kitenolojia duniani kote sekta binafsi imekua na imeonesha uzoefu mkubwa wa kimenejimenti kuliko sekta za umma,”.

Dkt.Jasinta Msamula kutoka Chuo Kikuu Mzumbe,amesisitiza juu ya umuhimu wa kuwa na nguvu kazi yenye uelewa wa masuala ya ubia na kubadili mfumo wa kibajeti ili kuweza kufikia malengo,kwani tafiti nyingi zinaonesha kuwa, kuimarisha serikali za mitaa kiuchumi ni njia ya haraka ya kukabilana na umaskini nchini.

Dkt.Ponsian Ntui,kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agoustino(SAUT),amesema kinachopaswa kufanyika ni kukuza sekta binafsi ya wazawa yenye nguvu ili kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.

“Tunahitaji kufanya mambo makubwa ikiwa ni pamoja na uchumi wa sasa kuweza kuhudumia sekta zote,kuwa na wataalamu wenye uwezo pamoja na mazingira bora ya ufanyaji biashara ili kuwavutia wawekezaji zaidi ndani,nje na kwenye Halmashauri,”amesema Dkt.Ntui.

Ambapo amependekeza kuwa kwa Mkoa wa Mwanza sekta binafsi kwa kushirikiana na serikali ya mtaa iwekeze katika fukwe za kisasa hali itakachochea uchumi wa Mkoa na taifa hivyo kufikia lengo.

“Kuwekeza katika maendeleo ya watu kwa kubadili mazingira ya afya na elimu kwa sekta binafsi kushirikiana na serikali ya mitaa kuanzisha mfuko wa afya na elimu,utakaosaidia kuboresha sekta hizo kwa wananchi wote,”.

Pia serikali ya mtaa kushirikiana na sekta binafsi kuhakikisha wanakuwa na teknolojia ya kisasa ya ukusanyaji wa taka mitaani kisha kuchakatwa na kutengeneza bidhaa nyingine ambayo itasaidia kulinda mazingira pamoja na kukuza uchumi.

“Mambo haya yote yanahitaji utashi na juhudi,sekta binafsi inahitaji ulinzi kwa kuwa na sera inayotabirika za kulinda,pia na kuwa na uchumi jumuishi ambao hautamuacha mtu nyuma ikiwemo wenye ulemavu katika kuzalisha na kutumia…..,Lazima kila mtu ashiriki katika kujenga na kuitengeneza keki ya taifa na kuila,”amesema Dkt.Ntui.

Baadhi ya washiriki wa kongamano juu ya nafasi ya ubia katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,lililofanyika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agoustino (SAUT) jijini Mwanza, lililoandaliwa na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi(PPPC) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu  cha Dar-es-Salaam,Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (REDET).

Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo cha Mtakatifu Agoustino(SAUT)Mwanza,Dkt.Delphine Kessy, amesema,ili kufanikisha hayo kuwe na chombo maalumu ambacho kitamsimamia  mbia na pia kifanye utafiti na kusaidia PPPC kuondoa makosa yaliojitokeza nyuma.

Dkt.Kessy,amesema kuwe  na mpango mzuri wa kufikia masoko ya nje ili kukuza uchumi wa taifa pamoja na kujenga uwezo wa wazalishaji  kufahamu bidhaa gani za kuzalisha na zenye soko pamoja na walaji kujua bidhaa gani wanunue.

Kwa upande wake, Mwanasheria Mkuu Mstaafu wa Serikali, Prof. Aderldus Kilangi,ameshauri kuwe na uchambuzi wa siasa uchumi kwenye faida na changamoto za dhana ya ubia ili tujifunze kutokana na historia katika hatua za kuboresha utekelezaji wake huku akitaka PPPC  ifanye utafiti wa changamoto ni nini katika miradi mbalimbali ya maendeleo.

“Ipo haja ya kupitia historia ya miradi ya PPP na kufanya utafiti wa kina kwanini tumekuwa na matatizo katika miradi,tuangalie sheria katika uwanda wake wote tusiangalie tu sheria ya PPP,”amesema Prof.Kilangi.

Baadhi ya washiriki wa kongamano juu ya nafasi ya ubia katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,lililofanyika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agoustino (SAUT) jijini Mwanza, lililoandaliwa na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi(PPPC) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu  cha Dar-es-Salaam,Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (REDET).

Hata hivyo baadhi ya wanafunzi walioshiriki katika kongamano hilo kutoka shule mbalimbali jijini Mwanza,wameomba elimu zaidi itolewe kuhusu uchumi na kutilia mkazo masomo ya biashara  kufundishwa kwa vitendo shuleni ambayo itaendana na uhalisia  pamoja na kuhakikisha wananchi wanaielewa vyema Dira ya Taifa na namna inavyopaswa kutekelezwa kwa vitendo.

Pia suala la teknolojia lipewe kipaumbele ili iweze kutumika katika kukuza sekta mbalimbali na kufikia uchumi imara pamoja na kuwa na chombo maalumu cha kusimamia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.